Polisi yathibitisha kumshikilia Mwenyekiti Bawacha Temeke

Polisi yathibitisha kumshikilia Mwenyekiti Bawacha Temeke

Muktasari:

  • Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) limesema mwenyekiti wao wa Jimbo la Temeke, Neema Mwakipesile anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa zaidi ya siku tano bila kuelezwa sababu yakushikiliwa kwake.

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limethibitisha kumshikilia Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) jimbo la Temeke, Neema Mwakipesile likieleza kuwa kiongozi huyo anashikiliwa kwa makosa aliyofanya katika Wilaya ya Kinondoni.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Mosi 2021, Kamanda wa Polisi mkoa wa Temeke, Richard Ngole amesema kuwa kiongozi huyo anashikiliwa baada ya kufanya makosa Wilaya ya Kinondoni.

Kamanda Ngole amesema “Ni kweli anashikiliwa na Jeshi la Polisi lakini makosa aliyafanya Kinondoni kwahiyo mtafute RPC wa Kinondoni anaweza kukueleza sababu inayomfanya ashikiliwe na Polisi”

Mapema leo Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) lilitoa taarifa kwa umma kuwa Neema Mwakipesile anashikiliwa na polisi kwa zaidi ya siku tano.  

Katika taarifa ya Bawacha ambayo ilisainiwa na Katibu Mkuu wa Bawacha Taifa, Catherine Ruge ilidai kuwa kiongozi wao anashikiliwa kwa zaidi ya siku tano sasa bila kuelezwa kosa lake wala kumfikisha mahakamani.

Taarifa hiyo imeeleza kwamba tukio hilo lilitanguliwa na tukio la kukamatwa kwa mume wake kwa madai kuwa angeachiwa pale ambapo mke wake angepatikana.

“Tangu kukamatwa kwake, Jeshi la Polisi limezuia asionane na ndugu zake, viongozi wa chama wala kupelekewa chakula kwa takribani siku tano sasa.” imesema taarifa hiyo ya Bawacha
Taarifa hiyo imeleleza kwamba hata pale Mwanasheria wa kiongozi huyo alipoenda kumuona alizuiliwa na alipowataka wampeleke mahakamani kama kuna kosa lolote amelifanya walijibu kuwa wao wanasubiri maelekezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) ambaye ndiye alitoa maagizo ya kushikiliwa kwake.