Polisi ‘yawatega’ Bawacha

Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam, SACP, Jumanne Muliro katika moja ya tukio akizungumza na waandishi wa habari. Picha na mtandao

What you need to know:

  • Wakati Baraza la wanawake Chadema (Bawacha) likitangaza kufanya maandamano Mei 11, kwa madai ya kupewa ulinzi, Jeshi la Polisi lashindwa kuthibitisha.

Dar es Salaam. Wakati Baraza la wanawake Chadema (Bawacha) likieleza kuwa wameruhusiwa kufanya maandamano kesho, Jeshi la Polisi Kanda Maalum limesema linasubiri siku hiyo ifike.

 Mei 7, mwaka huu Bawacha walipanga kufanya maandamano ya kushinikiza Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson kuwaondoa wabunge 19 ambao wameshafukuzwa uanachama na kupoteza sifa ya kuwa wabunge.

Hata hivyo maandamano hayo hayakufanyika, kwa kile walichodai wakati wakiendelea na maandalizi walipokea barua kutoka Jeshi la Polisi, ikiwaelekeza kuwa walifanya makosa kupeleka barua ofisini kwake.

Hata hivyo Mei 8, waliendeleza msimamo wao na kutangaza kufanya maandamano siku ya Alhamisi Mei 11 wakianzia Karume hadi, Ofisi ndogo za Bunge Dar es Salaam kabla ya kuelekea katika jiji la Mbeya na Dodoma ikiwa hatua hazijachukuliwa.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatano Mei 10, na Katibu Mkuu wa Bawacha Catherine Ruge, imeeleza kuwa Jeshi la Polisi limejibu barua yao ya taarifa ya kufanya maandamano siku ya kesho Mei 11 saa mbili asubuhi.

 “Wametuambia kwa kuwa maandamano yetu ni ya amani watakuwepo kuhakikisha kuna amani, utulivu na usalama, maandamano yetu yataanzia posta ya zamani pale kwenye bustani mpaka ofisi ndogo za bunge,” imeeleza taarifa hiyo.

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum, Muliro Jumanne kuthibitisha taarifa hizo za Bawacha endapo wameruhusiwa, alijibu tusubiri kesho ifike bila kuweka wazi kama jeshi hilo litatoa ulinzi au la.

Bawacha wamepanga kufanya maandamano hayo, wakati Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ikiwa imewaandikia barua ikiwashauri kusitisha kwa kuwa jambo wanalolilalamikia liko mahakamani.

Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza alikiri kuwaandikia barua Bawacha, akiwashauri kusitisha maandamano hayo kwa kuwa kesi bado ipo mahakamani.

Hili linafanyika ikiwa kesi ya wabunge hao kupinga kuvuliwa uanachama ikiendelea katika Mahakama Kuu, Masjala kuu ya Dar es Salaam na inatarajiwa kutajwa tena Mei 17, mwaka huu.