Profesa Janabi atoa angalizo ulaji wakati wa Krismasi

Muktasari:
- Profesa Janabi amesema chakula kina uwezo wa kumuondolea mtu ugonjwa au tatizo alilonalo, pia kinaweza kumsukuma kuingia katika magonjwa yasiyoambukiza.
Dar es Salaam. Kuelekea sikukuu za Krismasi na mwaka mpya, Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Mohamed Janabi ameshauri jamii kuzingatia mtindo bora wa maisha, akionya ulaji wa nyama na unywaji pombe kupitiliza.
Mbali ya hayo, amesema mtu anapojipa muda kati ya mlo mmoja na mwingine anausaidia mwili kujisafisha, hivyo kujiondoa kwenye hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza.
Profesa Janabi ambaye Desemba 8, 2024 aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mshauri wake wa masuala ya afya na tiba, ametoa wito huo leo Alhamisi Desemba 12, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari akitoa salamu zake za Krismasi kwa jamii.
Amesema chakula kina uwezo wa kumuondolea mtu ugonjwa au tatizo alilonalo, pia kinaweza kumsukuma kuingia katika magonjwa yasiyoambukiza.
“Mimi siyo mganga wa kienyeji wala mchungaji lakini naweza kufanya ugonjwa ukapotea, chakula kinaweza kukuondolea tatizo ulilonalo, ninaweza kumpa mgonjwa maelekezo kuhusu chakula na ugonjwa ukatoweka,” amesema.
Profesa Janabi amesema ni muhimu jamii ikajikita katika kujikinga kwa kuwa magonjwa hayo yana usumbufu na gharama kubwa kuyatibu.
“Tutoke kwenye mawazo ya kutibu magonjwa sugu, huamki asubuhi una hayo magonjwa bali unayatengeneza taratibu.
“Tunaenda kwenye msimu wa Krismasi na mwaka mpya kama ulaji utakuwa wa kupitiliza; mbege, mnazi, bia na nyama choma kwa wingi tunajijenga kwenda kufa. Unapokula kwa kujipa muda mwili unajisafisha ndiyo maana kufunga tunaambiwa kunasaidia kiafya,” amesema.
Amesema katika tafiti zilizofanyika duniani zimeonyesha ulaji wa mafuta ya wanyama na vyakula vya protini kama maziwa, nyama, mayai vinatakiwa kuwa wastani vikizidi ni hatari kwa afya.
Profesa Janabi amesema utafiti mkubwa kuwahi kufanyika nchini China na watafiti 650,000 kwa watu milioni 880 ulionyesha sehemu ya watu wenye uwezo waliokuwa na saratani walikuwa 16 kati ya watu 100,000 na kaya masikini alikuwa mtu mmoja kwa watu 100,000.
“Kwa kadri ulaji mkubwa wa kupitiliza wa vyakula vya protini, ndivyo unavyoongeza hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza. Wenye uzito uliozidi wajiangalie sana ulingane na urefu, ukiona una kilo zaidi ya 100 hata kama huumwi chunguza afya.”
“Tunashauri ulaji wa mboga za majani na matunda, kutembea pia. Watu wazima wengi hawawezi kutembea kwa sababu misuli haipo, nikinyanyua vyuma najenga misuli itanisaidia vizuri nikiwa na umri mkubwa. Namuomba Mungu nikifika miaka 80 niweze kufanya kazi kama mwenye miaka 60 siyo lazima niwe na six pack (hali ambayo misuli ya tumbo inaonekana kwa uwazi kama sehemu sita) hapana,” amesema.
Akizungumzia utoaji wa matibabu Muhimbili na Mloganzila, Profesa Janabi ambaye ni daktari bingwa mbobezi wa magonjwa ya moyo amesema wameendelea kuanzisha tiba mpya, ikiwemo upandikizaji figo kwa teknolojia ya kisasa zaidi.
“Idadi ya wagonjwa wanaokwenda nje imeendelea kushuka chini, tunapandikiza figo na Mloganzila tumeendelea zaidi. Pale aliyechangia anakaa saa 48 pekee, tumejifunza kwa Korea,” amesema.
Kuhusu upandikizaji uloto amesema wameshapandikiza wagonjwa 16.
Akizungumzia matibabu ya figo, amesema Muhimbili wanafanya usafishaji wa figo kwa wagonjwa 130 mpaka 150 kwa siku kuanzia saa 9:00 alfajiri mpaka saa 2:00 usiku.
Profesa Janabi amesema chanzo cha kufeli figo kwa asilimia 60 ni shinikizo la damu, ikifuatiwa na kisukari, unywaji holela wa dawa na vyanzo vingine.
Profesa Janabi amesema wamefanya marekebisho ya urembo kwa kinamama 23 ambao wameongeza na kupunguza maumbile.
Pia wamewawekea puto wagonjwa zaidi ya 200 ambao wote wanaendelea vizuri na wamepunguza tumbo kwa wagonjwa 11.
Amesema Afrika inachangia zaidi ya Dola bilioni 200 za Marekani kwa kutoa matibabu ya raia wake nje ya nchi, hivyo Muhimbili wamejipanga kuwa na wataalamu wa kutosha ili kuvutia tiba utalii.
“Katika fedha ambazo Afrika tunazitumia, nataka Tanzania tupate asilimia 10 pekee ya hao wagonjwa,” amesema.