Profesa Jay asimulia mateso aliyopitia siku 462 ICU, afichua kutobolewa koo
Muktasari:
- Jay aziweka kwenye wimbo siku 462 za ugonjwa wake, alivyoanza kuumwa hadi kulazwa ICU na ndugu walivyopinga na hatimaye kukubali uamuzi wa madaktari wa kumtoboa koo.
Dar es Salaam. ‘Nimepitia mengi katika siku 462 nilizokala kitandani, nimeona nimshukuru Mungu kwa ajili ya kipindi chote hicho na kunifanya niendelee kuwa hai hadi sasa na niwashukuru pia Watanzania kwa maombi na michango.’
Hivi ndivyo anavyosema mwanamuziki Joseph Haule maarufu kama Profesa Jay katika wimbo wake mpya alioupa jina la 462 ambapo amekuwa akisumbuliwa na tatizo la figo kwa takribani mwaka mmoja na miezi mitatu.
Profesa Jay ambaye kwa sasa afya yake inaendelea kuimarika ameachia wimbo huo unaoelezea maisha aliyopitia katika kipindi hicho cha ugonjwa kuanzia alivyoanza kuumwa hadi kupata nafuu.
Moja ya vitu alivyofichua msanii huyo ni pamoja na ndugu kukubali kutobolewa koo ili madaktari waweze kumtoa uchafu uliokuwa mwili mwake.
Katika wimbo huo aliomshirikisha mwanamuziki wa injili Walter Chilambo, Profesa Jay ameimba akieleza hatua kwa hatua ya ugonjwa wake hadi kulazwa kwenye wodi ya wagonjwa mahututi.
Baadhi ya mistari katika wimbo huo yamesikia akiimba, “Nilipumua kwa mashine hali ilikuwa mbaya, kila kona ya mwili nikiwekewa mawaya. Moyo wangu ulisimama madaktari wakasema hauwezi kufanya kazi tena, mapafu yaliyaa maji, figo zikawa na mchanga nilishindwa kupumua kabisa na kutangatanga.
Nikaanza kufanyiwa dialysis na kutolewa sumu mwilini, nikawa napewa chakula kupitia puani wakawa wanavuta uchafu kupitia mpira kinywani, wakasema haisaidii inabidi wanitoboe koo sauti yangu ndiyo mtaji na ndugu wakasema no. Uchafu ukaongeza nikashindwa hadi kukohoa ndugu na madaktari wakakubaliana kunitoboa,”amerap Profesa Jay kwenye wimbo huo.