Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Prof Jay: Madaktari wanatibu Mungu anaponya

Mwanasiasa na mwanamuziki nguli wa hip hop nchini, Joseph Haule

Dar es Salaam. Mwanasiasa na mwanamuziki nguli wa hip hop nchini, Joseph Haule ameelezea faraja aliyoipata baada ya mapokeo ya ujumbe wake kwa Watanzania.
Mwanamuziki huyo maarufu Profesa Jay, juzi aliweka ujumbe mtandaoni huku akisisitiza madaktari wanatibu lakini anaamini Mungu ndiye huponya.

Profesa Jay alisema hayo jana, alipozungumza na Mwananchi ikiwa ni takribani miezi 16 imepita tangu alipoanza kupigania maisha yake kitandani, Januari 2022.
Alisema mapokeo ya Watanzania yaliyoonekana kwa dakika chache tangu alivyoweka ujumbe wake kwa mara ya kwanza katika ukurasa wake wa Instagram na yamempa faraja inayomuimarisha zaidi kiafya.

“Kwa kweli imenionyesha picha kwamba watu wamenimiss sana, wananipenda na hadi wale ambao sikutegemea nimewaona wamepost, wengine wameandika maoni, wamenipigia, inaonyesha jinsi gani nimewaingia kwenye mioyo yao,” alisema Profesa Jay.

“Ninawashukuru wote walioleta mrejesho, kutoa maoni kwenye kurasa yangu. Mungu awabariki sana. Madaktari wanatibu tu, lakini Mungu ndiye anayeponya,” alisema nguli huyo aliyepokea maoni zaidi ya 19,000 kutoka kwa watu mbalimbali.

Profesa Jay, aliyekaa chumba cha uangalizi maalumu (ICU) kwa siku 127 sawa na miezi minne na wiki moja, aliandika ujumbe akitoa shukrani zake tangu alipoweka ujumbe wa mwisho Januari 23, 2022.

Katika ujumbe wake, mbunge huyo wa zamani wa Mikumi kupitia Chadema alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumlipia matibabu na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kwa jitihada alizozifanya akishirikiana na Serikali.

“Kwanza namshukuru sana Mungu aliye hai kwa uponyaji na kunipa nafasi nyingine ya kuendelea kuwa hai, hali yangu ilikuwa mbaya isiyoelezeka. Asante sana Mungu baba (nitakutukuza na kukusifu siku zote za maisha yangu),” alisema Profesa Jay.

“Kipekee namshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kwa kunigharamia matibabu yangu yote ya Muhimbili na nje ya nchi. Asante sana mama pamoja na Serikali yako yote, kwani viongozi wako wa chama na Serikali walikuwa wanapishana kila siku kuja kuniona na kunifariji.

“Mwenyekiti wa chama changu cha Chadema (Freeman Mbowe), wanachama na viongozi wote waandamizi wa chama, zaidi nawashukuru sana madaktari na manesi wote wa Muhimbili na kote nilikopitia kwa kunipa matibabu ya kiwango cha juu kwa zaidi ya mwaka mzima niliolala hapo Muhimbili.

“Hasa zile siku 127 za hatari nilizokuwa nimelazwa ICU, mlijitoa kwa uwezo wenu wote kuhakikisha kuwa mnaokoa uhai wangu, asanteni sana.”

Pia, aliwashukuru Watanzania waliojitolea kwa maombi na michango ya fedha, vyombo vya habari, watumishi wa Mungu walioongoza ibada maalumu ya kumuombea akiwataja wachungaji, masheikh na mapadri wote wa Kanisa Katoliki na familia yake.

Profesa Jay alianza kuumwa na kulazwa Januari 2022 na baadaye Februari 9 mwaka huo, familia iliruhusu kumchangia matibabu kabla Serikali haijachukua jukumu hilo Februari 11 na Juni 10 aliruhusiwa kutoka hospitalini.

Kupitia ujumbe wake wadau mbalimbali wakiwamo wananchi wa kawaida, viongozi wa kisiasa, kidini, wasanii na waigizaji mbalimbali walitoa maoni yao kupitia ukurasa wake wa Instagram na Twitter.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ameandika katika mtandao kuwa, “Mungu ni mwema. Kwetu sisi ni faraja kuona mgonjwa tunayemuhangaikia akitoka salama. Shukran nyingi kwa wataalamu wetu wa ndani. Asante Mungu.”

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ‘MwanaFA’ ameandika, “Mungu ni mwema.”

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa ameandika, “Mwenyezi Mungu aendelee kukuimarisha zaidi na zaidi. Tunasubiri mitulinga.”

Mwanasiasa na nguli wa Hip hop, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu Taita ameandika, “My Nigga! Mungu ni mwema sana. Na ataendelea kukutunza kwani ni wazi ana makusudi makubwa bado na wewe.”

Mwanamuziki kutoka Kenya, Akothee aliandika: “Mungu halali bro. Keep the Spirity Burning” huku Diamond Platnumz akiandika “Mungu ni Mwema.”

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Jokate Mwegelo aliandika, “Mungu mwema sana. Hongera mnooo kwa ujasiri na uvumilivu, wewe ni shujaa dada yangu (mke wa Profesa Jay) mpendwa.”

Mchekeshaji Idris Sultan ameandika, “Shule tunafunzwa kisha tunapata mtihani, kwenye maisha Mungu anatupa mtihani kisha tunaamua kama ni funzo au la. Allah amekunyanyua.”