Profesa Mkenda awashukia viongozi KNCU

Profesa Mkenda awashukia viongozi KNCU

Muktasari:

  • Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Profesa Adolf Mkenda ameonyesha kutoridhishwa na mwenendo wa chama kikuu cha ushirika Mkoa wa Kilimanjaro (KNCU) na kuwataka wanachama wake kuhakikisha wanachangua viongozi bora watakaokifufua chama hicho.

  

Moshi. Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Profesa Adolf Mkenda  ameonyesha kutoridhishwa na mwenendo wa chama kikuu cha ushirika Mkoa wa Kilimanjaro (KNCU) na kuwataka wanachama wake kuhakikisha wanachagua viongozi bora watakaokifufua chama hicho.

Ameeleza hayo leo Jumatatu Juni 28, 2021 wakati akizungumza kwenye mkutano mkuu wa 36 wa chama hicho.

Amebainisha kuwa aliomba uchaguzi wa viongozi wa bodi uliokuwa ufanyike leo uahirishwe ili kutoa muda kwa wanachama kutafakari namna ya kuwapata viongozi bora.

Amesema ilipo KNCU leo sipo inapostahili kuwepo na kueleza kuwa yanahitajika mabadiliko makubwa ili kukifufua chama hicho na kukirudisha kilipokuwa miaka ya nyuma.

"Natambua mlikuwa mfanye uchaguzi wa viongozi wa bodi katika mkutano huu, nilimuomba mrajisi wa vyama vya ushirika awaombe msifanye uchaguzi leo, na nia yangu ni ili mpate muda wa kutafakari na kuona namna ya kuwapata viongozi bora ambao wataivusha KNCU.”

"Ingekuwa mamlaka yangu ningesema mwaondoe viongozi wote wa bodi, lakini kwa kuwa ushirika ni mali ya wanachama, naomba wanachama mhakikishe siku ya uchaguzi, wanapatikana viongozi bora watakaowezesha chama hiki kusonga mbele na kurudi mahali pake," amesema.

Katika ufafanuzi wake amesema, “KNCU  ilitambulika nchini kama chama kikubwa na vyama vingine vilifika kujifunza, mlijenga chuo kikuu cha ushirika na hata shule ya sekondari ya Lyamungo, chama hiki kilibeba na kutoa  hata nuru ya ushirika nje ya Kilimanjaro  lakini leo hakuna kinachofanya."

"Tunahitaji mabadiliko makubwa katika chama hiki kwa kuwa kilikuwa chama kikubwa Afrika, kilijenga miradi mbalimbali na watu wengi walinufaika kupitia KNCU, leo kinafanya nini?”