Rais Mwinyi ateua Jaji Mkuu Zanzibar

Muktasari:

  • Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Mwinyi amewateua viongozi mbalimbali akiwemo Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Abdalla ambaye alikuwa anaikaimu nafasi hiyo.


  

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amewateua viongozi mbalimbali akiwemo Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Abdalla ambaye alikuwa anaikaimu nafasi hiyo.

Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Juni 24, 2022 na kusainiwa na Kaimu Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Mussa Haji Ali, imesema pia Rais Mwinyi amewateua majaji wengine watatu wa Mahakama Kuu ya Zanzibar.Uteuzi huo unaanza leo.

Walioteuliwa kuwa majaji ni pamoja na Salma Ali Hassan ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Mwingine ni Mohamed Ali Mohamed ambaye alikuwa Mrajisi wa Mahakama Kuu ya Zanzibar na Said Hassan Said ambaye alikuwa mwanasheria Mkuu katika Serikali ya Awamu ya Saba.

“Aidha Mheshimiwa Rais amewateua watendaji wafuatao; Salum Kassim Ali kuwa Mtakwimu Mkuu wa Serikali, kabla ya uteuzi huo Salum alikuwa Katibu Tawala Mkoa wa Kusini Unguja,” imesema

Mwingine aliyeteuliwa ni Dk Ali Salim Ali ambaye anakuwa mwenyekiti wa bodi ya Tume ya Ukimwi Zanzibar. Ali ni mshauri wa masuala ya Ukimwi katika Jumuiya ya Zapha.