Rais Samia afanya mazungumzo na Mkurugenzi wa IMF

Rais Samia afanya mazungumzo na Mkurugenzi wa IMF

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan leo amefanya mazungumzo kwa njia ya mtandao na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), Kristalina Georgieva kuhusu ushirikiano kati ya pande hizi mbili.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan leo amefanya mazungumzo kwa njia ya mtandao na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), Kristalina Georgieva kuhusu ushirikiano kati ya pande hizi mbili.

Rais Samia aliyekuwa ofisini kwake (Ikulu Chamwino) mkoani Dodoma amemshukuru Georgieva aliyekuwa nchini Marekani kwa ushirikiano na ufadhili mkubwa ambao IMF umeutoa nchini Tanzania na amemhakikishia kuwa serikali ya awamu ya sita itaendelea kukuza zaidi ushirikiano huo.

kwa lengo la kuendelea kujenga uchumi imara wa Tanzania.
Amemueleza juu ya hali ya uchumi wa Tanzania kwa sasa ambapo ukuaji wake umeshuka kutoka wastani wa asilimia 6.9 mwaka jana hadi asilimia 4.7 hivi sasa kutokana na changamoto za janga la ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona ambapo umeathiri sekta za uzalishaji na huduma za kijamii zikiwemo utalii, afya na kilimo.

“ Rais Samia amesema japo hali ya uchumi wa Tanzania bado ni nzuri, Serikali inahitaji kushirikiana zaidi na IMF kunusuru sekta zilizoathirika na janga la corona na kuendeleza miradi ya kimkakati ambayo utekelezaji wake unaendelea ikiwemo ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere katika mto Rufiji utakaozalisha megawati 2,115, reli ya kisasa na barabara na madaraja,” ilisema taarifa hiyo ya Ikulu.

Rais Samia, ambaye jana pia alifanya mazungumzo mapema na Rais wa zamani wa Nigeria, Olusegen Obasanjo, alisema pamoja na serikali kukabiliwa na changamoto, inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha uchumi ikiwemo kujenga mazingira mazuri ya kufanya biashara kama vile kuondoa dosari za kikodi na ardhi, kuimarisha utawala bora na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya nchi.

Kwa upande wake, Georgieva amempa pole Rais Samia kufuatia kifo cha Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli, aliyefariki Machi 17, mwaka huu.

Pia amempongeza kwa kupokea kijiti cha urais na amemhakikishia kuwa IMF ipo tayari kukuza zaidi ushirikiano wake na Tanzania kwa lengo la kuimarisha uchumi.

Georgieva amesema IMF ipo tayari kutoa ufadhili wa haraka kwa Tanzania kwa ajili ya kusaidia maeneo yaliyopata madhara makubwa ya kiuchumi kutokana na janga la corona zikiwemo sekta za utalii, afya, uzalishaji na huduma za kijamii na amebainisha kuwa shirika hilo litafanyia kazi mara moja
maombi ya mkopo nafuu kutoka Tanzania.

Ameongeza kuwa katika awamu ya pili, IMF imepanga kutumia Dola650 milioni kwa ajili ya kusaidia kwa dharura uchumi wa nchi mbalimbali zikiwemo nchi zinazoendelea zilizopatwa na madhara ya corona.

Kufuatia ahadi hiyo, Rais Samia amemuagiza Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,  Balozi Liberata Mulamula ambao wamehudhuria katika mazungumzo hayo kukamilisha haraka mchakato wa maandiko ya kuomba mkopo nafuu kutoka IMF ili fedha hizo zisaidie kuimarisha uchumi na kuboresha huduma za kijamii.