Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Samia athibitisha mmoja kugundulika na Marburg nchini

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema mtu mmoja amekutwa na maambukizi ya virusi vya Marburg (MVD) katika Wilaya ya Biharamuro mkoani Kagera.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema mtu mmoja amekutwa na maambukizi ya virusi vya Marburg (MVD) katika Wilaya ya Biharamuro mkoani wa Kagera, huku akisema nchi imefanikiwa kudhibiti maambukizi hayo.

Taarifa hiyo inakuja siku sita tangu Shirika la Afya Duniani (WHO) liweke wazi kuhusu watu wanane kufariki dunia kutokana na ugonjwa unaoshukiwa kuwa wa virusi vya Marburg mkoani humo.

Rais Samia ameyasema hayo leo Jumatatu, Januari 20, 2025 wakati alipozungumza na waandishi wa habari akiwa na  Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma.

Amesema nchi imefanikiwa kudhibiti ugonjwa huo mapema na mpaka sasa wahisiwa wote waliopimwa, hawajakutwa na maambukizi ya ugonjwa huo isipokuwa mmoja.

“Tanzania ipo salama, tunawakaribisha wageni wote wa ajili ya utalii na biashara,” amesema Rais Samia.

Akielezea suala hilo, amesema Serikali ilifanya jitihada kadhaa za haraka ikiwemo kutuma timu ya wataalamu kufanya uchunguzi wa suala hilo na kuchukua sampuli na kufanya vipimo vya maabara.

“Januari 11 tulituma timu ya wataalamu kuchunguza ili kuhakikisha umma unataarifiwa, vipimo vilichukuliwa na kupelekwa maabara ya Kabaile Kagera na baadaye kuja kufanyiwa uchunguzi katika maabara ya Taifa jijini Dar es Salaam.

“Ilibainika mtu mmoja amekutwa na maambukizi ya ugonjwa huo na wengine wamepimwa na kukutwa hawana maambukizi,” amesema.

Rais Samia amesema hiyo ni mara ya pili kwa nchi kupata maambukizi ya ugonjwa huo ambapo kwa mara ya kwanza ulibainika  Machi mwaka 2023 katika wilaya ya Bukoba.

“Mpaka kufikia Januari 20, 2025 sampuli 25 zilizopimwa maabara ni mgonjwa mmoja pekee amekutwa na maambukizi na hivyo kuifanya nchi kupata mlipuko huo kwa mara ya pili. Lakini mpaka sasa nchi ipo salama na hakuna maambukizi mengine yaliyobainika,” amesema Rais Samia.

Hata hivyo amesema kwa sasa bado wanaangalia chanzo cha mlipuko huo.

Kwa upande wake Mkurugenzi huyo wa WHO, Dk Tedros amesema Rais Samia amempa taarifa kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa Marburg nchini Tanzania uliotokea mkoani Kagera.

Katika kuunga mkono juhudi za kupambana na mlipuko huo, Dk Tedros amesema WHO inatoa Dola za Marekani 3,000,000 sawa na Sh7.5 bilioni.

“Kama ambavyo nchi ilifanikiwa kudhibiti miaka miwili iliyopita, tunaamini na sasa mtafanikisha kudhibiti ugonjwa huu. WHO inatoa dola za marekani milioni tatu kuhakikisha udhibiti na kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa,” amesema.

 “Tanzania ipo wazi kwa ajili ya shughuli zingine, kwani tayari wamefanikiwa kudhibiti ugonjwa huu mapema.”

Machi 16, 2023 Serikali kupitia Wizara ya Afya ilitangaza uwepo wa ugonjwa usiojulikana katika Kata ya Maruku na Kanyangereko, vijiji vya Bulinda na Butayaibega mkoani Kagera ambapo watu tisa walibainika kuathirika na Marburg.

WHO yapongeza sheria ya bima

Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo wa WHO ametumia fursa hiyo kuipongeza Tanzania kwa hatua kubwa ya kusaini sheria ya bima ya afya kwa wote mwaka 2023.

“Hii ni hatua kubwa katika kuifikia ‘Universal health coverage’ (huduma za afya kwa wote bila vikwazo vya kiuchumi) nawapongeza sana kwa hatua hii mliyoifikia mwaka 2023. Zaidi nimezungumza na Rais namna gani mtasonga mbele zaidi katika huduma hii,” amesema na kuongeza;

“Tumezungumza namna serikali inavyotakiwa kusimamia hili kuhakikisha mchakato huu unaanza mara moja, WHO inajivunia hili na kuhakikisha inaunga mkono juhudi hizi hasa katika kutoa mafunzo kwa watoa huduma ngazi ya jamii tunaoamini wanakwenda kutoa huduma moja kwa moja katika ngazi ya msingi,” amesema Dk Tedros.

Awali Rais Samia alieleza ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na WHO.

“Katika kikao chetu cha ndani, tumezungumza mengi na kuendeleza pale ambapo tumekuwa tukifanya kwa kipindi kirefu.

“Kwa pamoja tumefanikiwa kupunguza vifo vya wajawazito kwa asilimia 80 kutoka vifo 556 mwaka 2016/2017, mpaka kufikia vifo 104 mwaka 2022. Tuliwekeza zaidi katika huduma za dharura na vituo vya afya kuwa karibu na Watanzania na tumefanikiwa kwa asilimia 70 vituo vipo chini ya umbali wa kilomita 5,” amesema.

Pamoja na hayo alitaja uwepo wa changamoto katika kupunguza vifo vya watoto wachanga.

“Kwa sasa Serikali inapambana kuhakikisha huduma za watoto wachanga zinapatikana zaidi ikiwemo uanzishwaji wa wodi maalumu za watoto wachanga katika kila hospitali.

Pamoja na hayo amesema mwaka 2024 nchi ilifanikiwa kuzindua programu ya watoa huduma za afya ngazi ya jamii, ambao watafanya kazi katika ngazi za chini na tayari 37,000 wameajiriwa katika kusaidia kutoa huduma kwa jamii ikiwa ni sehemu ya kufikia bima ya afya kwa wote.

“Kufikia mwaka 2023 tulifanikiwa kuwa na sheria ya bima ya afya kwa wote na tayari tumeanza kufanya mchakato wa kuikamilisha.”