Rais Samia awapongeza Wakenya kwa uchaguzi wa amani

Muktasari:

Siku moja baada ya Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi (IEBC) ya Kenya, kumtangaza William Ruto kutoka Kenya Kwanza kuwa mshindi wa urais katika uchaguzi uliofanyika Agosti 9, 2022, Rais Samia Suluhu Hassan amewapongeza Wakenya kwa kufanya uchaguzi kwa amani na utulivu.

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi (IEBC) ya Kenya, kumtangaza William Ruto kutoka Kenya Kwanza kuwa mshindi wa urais katika uchaguzi uliofanyika Agosti 9, 2022, Rais Samia Suluhu Hassan amewapongeza Wakenya kwa kufanya uchaguzi kwa amani na utulivu.

Leo, Jumanne Agosti 16, 2022, Rais Samia ametuma salamu za pongezi hizo kupitia akaunti yake ya Twitter huku akiahidi kuwa Tanzania itaendeleza undugu wa kihistoria na Kenya.

"Ninapenda kuwapongeza kwa dhati wananchi wa Kenya kwa kushiriki uchaguzi wao mkuu kwa amani na utulivu, ambapo matokeo yake ni Dkt William Ruto kutangazwa kuwa Rais mteule wa Kenya. Tanzania itaendeleza undugu na ushirikiano wa Kihistoria na Kenya uliodumu miaka na mikaka" ameandika Rais Samia kwenye ukurasa wake wa Twitter leo.

Katika matokeo yaliyotangazwa jana na Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati, Ruto alishinda kwa kupata kura milioni 7.1 (asilimia 50.49) akifuatiwa na Raila Odinga aliyepata kura milioni 6.9 (asilimia 48.85), George Wajackoyah alipata kura 61,969 (asilimia 0. 44) na David Waihiga alipata kura 31,987 (asilimia 0.23).