Ramli zilivyochonganisha wananchi

Muktasari:

  • Wakati mwaka huu ukiwa unaelekea ukingoni, Mkoa wa Rukwa ulikuwa na habari nyingi, zikiwamo za wapiga ramli chonganishi maarufu kama ‘lambalamba.’


Rukwa. Wakati mwaka huu ukiwa unaelekea ukingoni, Mkoa wa Rukwa ulikuwa na habari nyingi, zikiwamo za wapiga ramli chonganishi maarufu kama ‘lambalamba.’

Wapiga ramli hawa walidaiwa ‘kuwateka wananchi kiimani’ wakiwaaminisha wanafichua wachawi na uchawi, hivyo kusababisha migogoro katika jamii.

‘Lambalamba’ ndio gumzo kila kona, vilio vya wananchi kutapeliwa, kuchonganishwa na ndugu na jamaa zao vimetawala.

Hali hiyo ilimlazimu Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Queen Sendiga kujitokeza hadharani kukemea uwepo wa kikundi hicho cha matapeli kinachosababisha taharuki kwenye jamii wakidai wanafichua washirikina.

Sendiga aliagiza waganga hao wasakwe, wakamatwe na wachukuliwe hatua za kisheria ikiwa ni njia mojawapo ya kuwadhibiti.


Ukweli kuhusu ‘lambalamba’

Ipo hivi, waganga hao wa jadi wasio na vibali wamekuwa wakiingia vijiji husika na kushirikiana na viongozi wakidai wanafichua wachawi na vitu vilivyofukiwa katika nyumba kishirikina.

Diwani wa viti maalumu, Zimba Mary alisema ‘lambalamba’ hao kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa vijiji wanadaiwa kutumia msimu wa kilimo, nyakati ambazo watu wapo shambani, kuchimba mashimo kando ya nyumba zao na kufukia pembe na vitu vingine vya kishirikina na kurejea nyakati za msimu wa mavuno wakidai kufichua uchawi katika nyumba hizo.

Mary alisema wanaporejea kipindi cha mavuno, waganga hao huwa wanataka wapewe fedha taslimu au mali kama mazao na mifugo wakidai wanafichua uchawi na baada ya makubaliano huenda kwenye maeneo waliyofukia vitu hivyo na kuvifukua.

Alisema baada ya kufukua vitu hivyo wamekuwa wakimtaja mtu yeyote katika kijiji hicho kwamba ndiye anawafanyia ushirikina wenzake, kitu ambacho sio sahihi.

Mary alisema uchonganishi huo umekuwa ukipokewa kwa sura mbili, huku wengine wakiamini na kuendelea kuwachangia fedha na mali nyingine, huku wale watuhumiwa wakilalamika kutokana na kusingiziwa washirikina.

Hata hivyo, Sendiga alisema wale wanaowaamini ‘lambalamba’ wamekuwa wakiwakabidhi watoto wao wa kike ili wawe wanashiriki nao ngono kipindi wanapokuwa kijijini wakifanya kazi yao.


Athari za ‘lambalamba’

Hivi karibuni iliripotiwa baadhi wananchi wameanza kuwakataa watumishi katika Kiijiji cha Serengoma kwa madai ya imani za kishirikina.

Tukio kama hilo pia, lilitokea Kijiji cha Zyangoma baada ya wananchi kuandika mabango ya kuwataka walimu watatu kuondoka kijijini kwa kugoma nyumba zao kufanyiwa msako wa tunguli za uchawi.

Kutokana na kushamiri kwa matukio hayo, hasa Wilaya ya Kalambo, uongozi wa wilaya na mkoa umeendelea kutoa elimu kwa jamii kutoamini vitendo vya ushirikina, huku Jeshi la Polisi likiwatia nguvuni wale wanaojihusisha na vitendo hivyo.


Lambalamba wanaswa Rukwa

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Theopista Mallya, ‘lambalamba’ wapatao 189 wamekatwa katika wilaya zote za mkoa huo, huku kesi zilizofunguliwa mahakamani ni 53.

“Tunawafungulia kesi za kufanya shughuli za uganga wa jadi pasipo kibali,” alisema Kamanda.


Wananchi wazungumza

Mmoja wa wakazi wa Kata ya Mambwe Kenya, Edwin Msipi alisema waganga hao wa jadi ni kero kwa wananchi kutokana na kuwatapeli fedha na mali nyingine, yakiwamo mazao na mifugo kwa madai wanafichua uchawi uliofukiwa kando ya nyumba zao.

Msipi alishauri Serikali iendelee kuwadhibiti waganga hao ili kurejesha amani katika maeneo yao kwa kuwa wamesababisha uhusiano kati ya familia, ndugu na jamaa kuharibika kutokana na kupiga ramli chonganishi.

Mkazi mwingine wa kata hiyo, Maufi Mzindakaya alisema Serikali pamoja na kutoamini ushirikina, inapaswa kutumia vyombo vyake vya ulinzi na usalama kuwadhibiti ‘lambalamba’ kwa kuwa wanakiuka sheria na taratibu za nchi na kuchochea uvunjifu wa amani.


Viongozi wa dini wanena

Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Ziwa Tanganyika, Ambele Mwaipopo alisema wao kama viongozi wa dini tayari wametoa tamko kupinga vitendo hivyo vya imani za kishirikina.

“Wanachofanya ‘lambalamba’ ni udanganyifu, uchonganishi na kuleta fitina katika jamii na wanarudisha nyuma maendeleo ya jamii na mkoa kwa jumla, hivyo hawapaswi kufumbiwa macho,” alisema Mwaipopo.

Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Rukwa, Ustadhi Mohammed Adam alisema kinachofanywa na ‘lambalamba’ ni kukiuka sheria za nchi na vitabu vya dini vinavyopiga marufuku vitendo vya kufanya ramli chonganishi, hivyo hatua kali zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya matapeli hao.

Alisema pamoja na viongozi wa dini kuendelea kutoa elimu kanisani na msikitini, ni vyema pia Serikali ya mkoa kupitia Jeshi la Polisi kuwa na operesheni endelevu ya kuwasaka ‘lambalamba’ hao.