RC Geita ampa mkandarasi siku 30 kumaliza ujenzi chuo

Friday May 20 2022
RC pc
By REHEMA MATOWO

Geita. Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule amemtaka mkandarasi anaejenga chuo cha Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) Geita kufanya kazi usiku na mchana na kukamilisha mradi huo ndani ya siku 30.

Akizungumza leo Mei 20 mara baada ya kutembelea na kukagua mradi huo ambao hadi sasa umekamilika kwa asilimia 57, RC Senyamule ameeleza kukerwa kuona kazi zinafanywa kwa taratibu wakati kazi inatakiwa ikamilike ndani ya mwezi huu.

Amesema Serikali imeamua kuuendeleza mradi huo baada ya kusimama kwa zaidi ya miaka mitatu kutokana na upungufu ya mkandarasi kiutendaji.

“Mradi huu ulikua umesimama na Serikali sasa imeamua kuujenga kwa kutumia force account na unajengwa kwa fedha za Uviko 19 kama mnavyojua mwisho wa fedha hizi ni Juni 30 miradi yote iwe imekamilika.

“Sipo tayari kuona mkoa wangu unakwamisha nchi kupata fedha nyingine,” amesema Senyamule.

Amemtaka mkandarasi mshauri kusimamia vema mradi huo ifikapo Juni 20 akabidhi mradi ukiwa umekamilika.

Advertisement

“Hapa fundi yupo mmoja kazi hii ni kubwa sio ya fundi mmoja hata kama tunajenga kwa force Account, lazima pawe na mafundi na vibarua wa kutosha. Geita wapo mafundi wengi na wanataka kazi sioni sababu ya kuwa na watu wachache mnajenga jengo moja moja wakati muda umeisha,” alisema Senyamule

Akieleza sababau ya kuchelewa kwa mradi huo unaojengwa kwa gharama ya Sh4.2 bilioni, msanifu majengo na mhandisi mshauri kutoka chuo cha ufundi Arusha, Jonny Idelya amesema mvua zilizokuwa zikinyesha ndiyo sababu.

“Wakati wa mvua eneo hili lilijaa maji tukashindwa kufanya kazi lakini hata magari yaliyokuwa yanabeba vifaa yalishindwa kuingiza vifaa kutokana na tope.

“Sababu nyingine ni ucheleweshwaji wa malighafi kutoka viwandani hadi sasa yapo machuma hayajafika unatoa oda inakaa zaidi ya miezi miwili hujapata,” amesema Idelya

Advertisement