RC Homera ataka operesheni kukabili ufugaji holela

Mkuu wa mkoa wa Mbeya Juma Homera akipanda mti ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa zoezi la upandaji miti Wilaya ya Chunya ambapo kiwilaya limezinduliwa  kwenye eneo la jengo jipya la Halmshauri ya Wilaya ya Chunya,picha na Mary Mwaisenye

What you need to know:

  • Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera ameagiza kufanyika operesheni kwenye maeneo yote yaliyovamiwa na wafugaji ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira.

Chunya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema kuna haja ya kufanya operesheni kwenye maeneo yote yaliyovamiwa na wafugaji ili kukabiliana na mabadiliko uharibifu wa mazingira.

Homera ametoa kauli hiyo Februari 2, 2023 katika uzinduzi wa upandaji miti Wilaya ya Chunya ambapo amesema wafugaji wote waliovamia maeneo yaliyohifadhiwa pamoja na maeneo ya vyanzo vya maji Serikali itahakikisha inawaondoa ili kunusuru wilaya kukabiliwa na ukame.

Amesema pamoja na juhudi za upandaji miti zinazofanywa na Serikali bado kuna changamoto kubwa ya uharibifu wa mazingira kutokana na uingizwaji holela wa mifugo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa.

“Mifugo hiyo inatoka maeneo totauti yanayopakana na Wilaya ya Chunya hivyo kuna haja ya kufanya operesheni ili kuondoa wavamizi wote,” amesema Homera.

Aidha, Homera amepongeza ofisini ya Misitu Wilaya ya Chunya kwa namna wanavyoshirikiana na wadau mbalimbali wanaojihusisha na kilimo cha tumbaku na uchimbaji wa madini ya dhahabu katika uoteshaji miche pamoja na kuisimamia.

Akitoa taarifa ya upandaji miti wa wilaya hiyo kwa upande wake Ofisa Misitu Wilaya, Rehema Mwabulambo amesema katika kutekeleza kampeni ya upandaji miti msimu wa mwaka 2022/2023 wamejipanga kupanda miti zaidi 5.7 milioni kwenye shule za msingi na sekondari, taasisi za dini, magereza, vyanzo vya maji, pamoja na makazi ya watu.

Mwabulambo amesema katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi halmashauri imekuwa ikisimamia upandaji miti maeneo totauti ya wilaya ambapo amesema kwa wastani hekta 200-250 hupandwa miti kila mwaka.

Aidha, amebainisha changamoto wanazokutanazo Kuwa ni uhamiaji holela kwenye maeneo ya wazi, hifadhi za misitu, vyanzo vya maji, ufunguaji wa mashamba unaosababishwa na wakulima na wafugaji kutoka mikoa jirani.