RC Kilimanjaro ahimiza utunzaji mazingira shuleni
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kisare Makori (katikati) akishuhudia Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya St Mary Goreti, Sr Clementina Kachweka (kulia) akipokea Lipa Namba ya Tigo itakayotumika kupokea michango kwa ajili ya harambee ya shule hiyo, kutoka kwa Meneja Mauzo wa Tigo, Silas Mkuyu (wa pili kushoto). Wengine kutoka kushoto ni Meneja Msaidizi wa shule, Moses Silayo na Mwenyekiti wa Bodi, Injinia Theonis Bebwa.
Muktasari:
- Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu ameipongeza shule ya sekondari ya St Maria Goreti iliyoko Moshi, kwa ubunifu na juhudi katika kuboresha na kutunza mazingira.
Kilimanjaro. Serikali mkoani hapa imeupongeza uongozi wa Shule ya Sekondari ya St Maria Goreti iliyoko Moshi, kwa ubunifu na juhudi katika kuboresha na kutunza mazingira sambamba na kuboresha afya ndani ya jamii.
Pongezi hizo zimetolewa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu katika taarifa iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa wilaya ya Moshi, Kisare Makori, wakati wa hafla ya uzinduzi wa harambee ya maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa shule hiyo.
“Mbali na kazi nzuri mnayofanya katika kutoa elimu ambayo imebadilisha maisha ya watu wengi, pia taarifa zinaonyesha ya kuwa mmetoa na mnaendelea kutoa michango mingi katika kuboresha mazingira na afya ndani ya jamii, hili hatuna budi kuwapongeza,” amesema.
Babu amesema kwa kufanya yote hayo shule hiyo inaunga mkono juhudi za Serikali za kujenga jamii iliyo bora kielimu na kiafya.
“Juhudi zenu hizi hazina budi kuungwa mkono na wadau wengine kutokana na ukweli ya kuwa elimu na afya njema ni muhimu kwa wanadamu ambao wana kazi ya kukabiliana na changamoto za kimaisha kila siku.”
Babu pia amezipongeza taasisi za dini kwa michango inayotoa kupitia sekta mbalimbali zikiwamo za elimu na afya jambo ambalo lililochangia wananchi wengi kupata huduma nzuri na endelevu kupitia taasisi hizo.
Babu ametoa rai kwa wadau mbalimbali wa maendeleo na wanachi wote kwa ujumla kutoa ushiriakiano wao wa dhati kwa uongozi wa Maria Goreti ili kufanikisha sherehe yao. “Nina uhakika kuna wadau wengi huko nje ikiwamo wote waliosoma katika shule hii na pindi tu wakiskia taarifa hizi, watajitokeza kuchangia kw anguvu zote,” amesema.
Katika taarifa yake Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Maria Goreti Sr Clementina Kachweka amesema maadhimisho hayo ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa shule hiyo yanatarajiwa kufanyika Septemba, mwakani.
“Kuelekea maadhimisho hayo tunatarajia kufanya ukarabati mkubwa na ndiyo haswa sababu ya uzinduzi rasmi wa Harambee ili kupata fedha kwa ajili ya shughuli za ukarabati huo”, amesema
“Pia kuelekea jubilee tumeandaa shughuli malimbali ambazo tutazifanya kama shule kwa kushirikiana na jamii kwa ujumla, ambazo ni pamoja na upandaji miti kwa ajili ya kutunza vyanzo vya maji; hili pia litakuwa ni kuunga mkono ofisi yako ambayo imekuwa mstari wa mbele katika kutunza mazingira”.
Amezitaja shughuli nyingine kuwa ni pamoja na kuwa na kampeni ya afya kwa kuachangia damu na matembezi ya hisani yatakayolenga kukusanya fedha kwa ajili ya shughuli zinazohusiana na maadhimisho hayo.
“Matarajio yetu ni kukusanya jumla ya Sh600 milioni kwa ajili ya ukarabati wa shule yote kwa jumla; tayari kwa kuanzia tumeshawaarifu wazazi wenye wanafunzi wanaosoma shuleni hapa kuhusu mipango yetu hii,”amesema.
Amesema matumaini yake ni kuwa uongozi wa Bodi na ule wa shule hiyo utapata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wanafunzi waliosoma shuleni hapo ambao ni zaidi ya 10,000 walioko ndani na nje ya nchi jambo litakalofanikisha shughuli hizo za jubilei.
Shughuli hizi za kuelekea jubilee ya St Mary Goreti zinaratibiwa na Executive Solutions Limited moja ya makampuni yanayoongoza katika kuandaa matukio na kuratibu maswala ya habari na mawasiliano.