RC Makalla awaahidi wafanyabiashara kituo cha huduma ya pamoja

Wednesday August 04 2021
makkallapic

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla

By Bakari Kiango

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amesema kuanzia Septemba Mosi 2021, kutakuwa na kituo cha kutolea huduma ya pamoja (One  stop center), kitakachosimamiwa na uongozi wa mkoa huo ili kurahisisha shughuli za biashara kwa wafanyabiashara na wawekezaji.

Makalla ameeleza hayo leo Jumatano, Agosti 4, 2021 wakati akifungua kikao cha baraza la biashara la mkoa huo, kilichowashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara, wakurugenzi na wakuu wa wilayani za Dar es Salaam.

Katika maelezo yake, Makalla amewahakikishia wajumbe wa baraza hilo, Serikali ya mkoa huo imejipanga vyema kuhakikisha wafanyabiashara na wanaotaka kuwekeza ndani ya jiji la Dar es Salaam wanafanya shughuli kwa ufanisi bila urasimu wa aina yoyote.

"Kuanzia Septemba Mosi tutakuwa na one stop center wapi itakuwa tutawajulisha, tunataka huduma zote zipatikane sehemu moja. Kituo hiki kitakuwa chini ya mkoa wa Dar es Salaam na wafanyabiashara na wawekezaji watapata huduma katika sehemu moja hawatasumbuka," amesema Makalla.

Naye katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Hassan Rugwa amewaambia wajumbe wa baraza hilo, viongozi wa mkoa huo wanatambua kazi kubwa inayowafanywa na wafanyabiashara wa Dar es Salaam na aliwaahidi kuwapa ushirikiano wakati wote.

"Viongozi wa Dar es Salaam tuna wajibu mkubwa wa kuhakikisha  baraza hili linatekeleza majukumu yake kwa ufanisi, tunawaahidi kuwapa ushirikiano wa karibu.Tutakuwa tunakutana tunakutana kwa kila makundi kujadili changamoto zinazowakabili," amesema Rugwa.

Advertisement
Advertisement