RC Makalla: Wafanyabiashara waende katika maeneo waliyopangiwa

Muktasari:
- Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amewataka wafanyabiashara waliorudi katika maeneo waliyokatazwa kufanya biashara kuondoka mara moja.
Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amewataka wafanyabiashara waliorudi katika maeneo waliyokatazwa kufanya biashara kuondoka mara moja.
Makalla ametoa agizo hilo leo jijini Dar es Salaam wakati akiendesha zoezi la usafi katika soko kuu la Kariakoo ambapo amesema wapo tayari kuwapokea wale wote waliokosa maeneo ya kufanya biashara na kuwasaidia.
Amesema kwa sasa wanataka maeneo yote yaliyokatazwa kufanyabiashara kuwa wazi na wafanyabiashara wote waende katika maeneo waliyopangiwa.
"Wafanyabiashara wote waliorudi katika maeneo waliyoondolewa wanapaswa kuondoka, niwakumbushe tu hairuhusiwi kufanya biashara kwenye njia za wapita kwa miguu, usifanye biashara kukinga duka la mwenzako, kwenye maeneo ya hifadhi za barabara na usijenge kibanda juu ya mfereji na katika shule.
"Mambo yako wazi ila kuna baadhi ya watu wanajaribu sana, wapo wanaowadanganya wafanyabiashara kurudi katika maeneo tuliyokataza, tena nimeambiwa mtaa wa Congo hapa Kariakoo na maeneo mengine kuna watu wanadanganywa na wanaweka biashara nimewaambia waondoke kama tulivyokubaliana, tutaweka askari maeneo yote watakaolinda saa 24," amesema Makalla
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng'wilabuzu Ludigija amesema mfanyabiashara yeyote atakayefanya biashara katika maeneo ambayo yamekatazwa atachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.