RC Mtaka aahidi kuipaisha Njombe kielimu

Mkuu wa Mkoa wa Njombe (RC), Anthony Mtaka (kushoto) akikabidhiwa nyaraka na aliyekuwa mkuu wa mkoa huo, Waziri Kindamba ambaye amehamishiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe.

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Njombe (RC), Anthony Mtaka ametua mkoa humo akitokea Dodoma alikokuwa anahudumu. Ameahidi kuupaisha mkoa huo kielimu na kiuchumi.

 
 

Njombe. Mkuu wa Mkoa wa Njombe (RC), Anthony Mtaka amesema atahakikisha mkoa huo unaongoza kitaifa kwenye matokeo ya mitihani ya darasa la nne mpaka kidato cha nne.

Kauli hiyo ameitoa mara baada ya makabidhiano ya ofisi ya mkuu wa mkoa wa Njombe katika hafla iliyofanyika mkoani humo jana Ijumaa, Agosti 5, 2022.

Alisema ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, atahakikisha mkoa huo kwa upande wa elimu unaongoza kwenye matokeo ya mitihani ya taifa kuanzia darasa la nne mpaka kidato cha nne jambo ambalo linawezekana.

Alisema mwanafunzi tangu anaanza kidato cha kwanza masomo ya sayansi anafanya vibaya hivyo hakuna miujiza ambayo ataifanya ndani ya miezi minne na kufaulu mtihani wa kidato cha nne.

Alisema hakuna sababu ya kumbebesha mwanafunzi masomo kumi na moja wakati matokeo yake ya kidato cha tatu kwenda cha nne alipata sifuri.

Aliwaagiza maofisa elimu wa shule za sekondari kuangalia wanafunzi wote waliokuwa kidato cha tatu na kupata matokeo ya sifuri na sasa wapo kidato cha nne wawafundishe masomo matano pekee ambayo ni Kiswahili, Kingereza, jiografia, Civics na Historia kwani hakuna sababu ya mwanafunzi kupata sifuri.

"Mtoto afundishwe masomo matano tu anasoma vizuri na anayapenda unamtoa mtoto kwenye ziro na anapata cheti chake cha kidato cha nne hasa ukizingatia waajiri wengi leo sifa ya kwanza kuwa na cheti cha kidato cha nne," alisema Mtaka aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma

Alisema kipaumbele chake cha pili ni uchumi wa watu ambapo alizitaka halmashauri kuwekeza na kuacha kutegemea mapato kutoka kwenye makusanyo ya watu wengine.

"Kama tunaamini ngano ni biashara nzuri tunatarajia kwenye halmashauri mkurugenzi atapima ardhi kisha weka kilimo cha ngano na hata kama haulimi pangisha wakulima wakati miundo mbinu kama barabara,umeme, maji na jenga nyumba kwa ajili ya idara ya kilimo," alisema Mtaka.

Alisema mkoa wa Njombe ni tajiri hivyo ni kuweka malengo tu kwa kipindi fulani mkoa huo unakuwa hauna wanachama wanategemea fedha kutoka kwenye mfuko wa tasaf.

Alimuahidi mkuu wa mkoa wa Songwe, Waziri Kindamba kuwa atatekeleza yale yote ambayo alitamani kuyafanya wakati yupo Njombe kabla ya kuhamishiwa mkoa mwingine.

Mkuu wa mkoa wa Songwe, Waziri Kindamba kabla ya kumkabidhi ofisi mkuu mpya wa mkoa wa Njombe Anthony Mtaka alisema yapo mambo sita ambayo angetamani kuona yanafanyika licha ya kuhamishwa kwake na kwenda mkoa Songwe.

Alitaja mambo hayo kuwa ni ujenzi wa uwanja wa ndege, ujenzi wa kiwanda cha kukamua mafuta ya Parachichi, uwekezaji wa kilimo cha Soya, uanzishwaji wa mradi wa samaki pamoja na suala la Liganga na Mchuchuma ambalo lilianza tangu kipindi cha serikali ya awamu ya tatu.

"Hayo mambo sita nilipanga yamature kabla ya mwezi Desemba mwaka huu kama mungu akikusaidia yanaweza kufanyika kabla" alisema Kindamba.

Naye Katibu tawala mkoa wa Njombe, Judica Omary alimshukuru Waziri Kindamba mkuu wa mkoa wa Songwe kwa ushirikiano aliouonyesha wakati akiwa mkuu wa mkoa wa Njombe licha kudumu kwa kipindi kifupi cha miezi minne.

Aliwataka wananchi wa mkoa wa Njombe kuonyesha ushirikiano kwa mkuu mpya wa mkoa Anthony Mtaka ili kumuwezesha kutimiza majukumu yake.

"Mimi nitashirikiana pamoja nanyi tumuwezeshe mheshimiwa mkuu wa mkoa ambaye amekuja tufanye nae kazi kwa karibu nikiamini mkoa wetu wa Njombe utaendelea kuwa mstari wa mbele," alisema Judica.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Njombe Jassery Mwamala alisema kwa muda ambao Waziri Kindamba amefanya kazi mkoani hapa wananchi wameona juhudi zake za kuleta maendeleo pamoja na kudumu kwa muda mfupi mkoa umesonga mbele.

Alisema Mtaka alipokuwa Simiyu alifanya jambo moja kubwa la kuanzisha maonyesho ya biashara ambayo yalifanya mkoa huo kusonga mbele.

"Tunaamini hata Njombe utayafanya hayo ambayo umeyazungumza kwenye hotuba yako tunakutarajia sana," alisema Mwamala.