Rc Nawanda ataka busara itumike maamuzi ya kutaifisha mifugo

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dk Yahya Nawanda akizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Katiba na Sheria Dk Pindi Chana

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk Yahya Nawanda ameiomba Ofisi ya Taifa ya  Mashtaka Mkoa wa Simiyu kutumia busara wakati wa maamuzi ya kutaifisha mifugo inayokamatwa ndani ya hifadhi na badala yake wawapige faini pamoja na kutoa elimu kwa wafugaji wanaoishi jirani na hifadhi za wanyamapori.

Bariadi. Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk Yahya Nawanda ameiomba Ofisi ya Taifa ya  Mashtaka Mkoa wa Simiyu kutumia busara wakati wa maamuzi ya kutaifisha mifugo inayokamatwa ndani ya hifadhi na badala yake wawapige faini pamoja na kutoa elimu kwa wafugaji wanaoishi jirani na hifadhi za wanyamapori.

Akiwa ameambatana na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Pindi Chana katika ziara ya kuitembelea ofisi hiyo leo Septemba 19, 2023 amesema changamoto ya kuingiza mifungo katika maeneo ya hifadhi hasa Serengeti ni kubwa.

"Tunaendelea kuwaomba waendesha mashtaka kutumia mbinu zinazofaa kuamua mashauri haya, kuwalipisha faini ni nzuri lakini kutaifisha mifugo inaleta migogoro, tunaomba ofisi yako iangalie njia mbadala ili tusitengeneze migogoro mingi kwenye jamii," amesema Nawanda

Ameongeza kuwa ofisi yake ipo tayari kuwezesha zoezi la utoaji elimu kwa wananchi wanaoishi maeneo ya pembeni ya hifadhi kwa kushirikiana na wanasheria wa Tawa pamoja na Tanapa ili kuwasaidia wananchi kuelewa mipaka yao katika maeneo ya hifadhi.

"Kumekuwa na malalamiko pia kuwa ng'ombe wanaokamatwa sio wale wanaorudishwa hilo mlitazame pia, tuhakikishe wananchi wanapata elimu ili yule atakayerudia baada ya kupata elimu hatua zaidi zichukuliwe dhidi yake," amesema Nawanda

Awali akitoa taarifa kwa waziri, Mwendesha Mashtaka wa Mkoa wa Simiyu, Shabani Mwegole amesema Desemba 2022 hadi April 2023 waliamua mashauri nane ya kuingiza mifugo hifadhini kati ya wafugaji na wahifadhi.

"Hatua  iliyochukuliwa ni kutaifisha mifugo hiyo lakini kwa kipindi cha mwezi Mei hadi June mashauri nane yameamriwa  ambapo watuhumiwa  wamewalipishwa faini," amesema Mwegole

Akizungumza baada ya kupokea taarifa ya ofisi hiyo Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Pindi Chana amewataka wananchi kuzingatia sheria na kutoivunja.

"Wakati umefika wa kufuata sheria inatakiwa tufuge bila kuingilia mashamba ya mtu wala hifadhi kama malisho hakuna Serikali za vijiji vikae vijadili vinapeleka wapi mifugo" amesema Dk Chana

Ameongeza kuwa nchi ipo kwenye utawala wa kisheria mtu anapofanya kosa sheria inachukua mkondo wake kwahiyo ni vyema kila mmoja kuelewa mipaka yake ili kukwepa kukiuka sheria.