RC Njombe awaagiza polisi kuzuia mikusanyiko ili kudhibiti corona

Wednesday August 04 2021
By Seif Jumanne

Njombe. Mkuu wa mkoa wa Njombe mhandisi Marwa Rubirya amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe kuendeleza oparesheni ili kuhakikisha hakuna mikusanyiko isiyo ya lazima na wananchi wanachukua tahadhari zote za kujikinga na corona hususani kwa kuvaa barakoa.

Agizo hilo amelitoa leo wakati akizindua rasmi chanjo ya corona kwa mara ya kwanza katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Njombe iliyofanyika mkoani hapa.

Amesema ni muhimu kuhakikisha maeneo yote ya mikusanyiko yanafanyiwa ukaguzi ili wananchi wavae barakoa wakati wote katika kukabiliana na ugonjwa huo.

"Nimeshatoa maelekezo kwa kamanda wa polisi wa mkoa tuendelee kulisimamia hili kwenye vituo vya mabasi wasafiri wote lazima wavae barakoa," amesema Rubirya.

Amesema ni ukweli usiyo na kificho kuwa unapokaa kwenye kiti hakuna mwenye uhakika na afya ya mwenzake hivyo ni muhimu kuchukua tahadhari kwa kuvaa barakoa.

Awali katibu tawala wa mkoa wa Njombe Judica Omary amesema tayari katika vituo vyote 19 vya mkoa wa Njombe vimeshapatiwa dozi za chanjo hiyo na zoezi linaendelea.

Advertisement

"Tumepokea chanjo zetu tulizopangiwa kama mkoa elfu thelathini ambazo mpaka leo zimeshasambazwa katika vituo vyote vya afya" amesema Judica.

Mganga mkuu wa mkoa wa Njombe Dkt.Zabron Masatu amewatoa hofu wananchi wanaopata chanjo hiyo kuwa ni salama na mpaka sasa hakuna aliyepata tatizo kutokana na kupata chanjo hiyo.

"Ukishachanja unaendelea na maisha ya kawaida unaweza ukapata maumivu kidogo na ukipata kahoma unakunywa hata Panadol lakini hakuna kitu Cha kukuzuia labda ukichanja usifanye kitu fulani" amesema Dkt Masatu.

Kamanda wa polisi mkoa wa Njombe Hamisi Issah amesema jeshi hilo bado linaendelea kutoa elimu katika maeneo mbalimbali yenye mikusanyiko ili kukabiliana na janga hili.

"Hizi elimu zinaendelea kutolewa ili maeneo hayo wananchi wapata uelewa kuhusu usalama wao na jinsi ya kujikinga kwani sasahivi hili jambo.limekuwa gumu ni lazima vyombo vya dola viingilie kati," amesema Issah.

Advertisement