RC Shigella atoa maagizo jumuiya za watumiaji maji Geita

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella akiwasha moja ya pikipiki zilizotolewa na Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) kwa mameneja wa wilaya na wale wa jumuiya zilizotolewa kuwawezesha kufika kwa wananchi na kuwapa huduma ya maji bila vikwazo.

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Geita (RC), Martin Shigella amezitaka jumuiya za watumia maji kuheshimu kanuni, miongozo na taratibu zilizotolewa na Serikali kwenye bei ya maji zilizoanza kutumika Agosti 1, 2022.

Geita. Mkuu wa Mkoa wa Geita (RC), Martin Shigella amezitaka jumuiya za watumia maji kuheshimu kanuni, miongozo na taratibu zilizotolewa na Serikali kwenye bei ya maji zilizoanza kutumika Agosti 1, 2022.

 RC huyo amesema hayo leo Alhamisi Agosti 11, 2022 mjini Geita wakati akikabidhi pikipiki nane kwa mameneja wilaya zilizopo mkoani humo pamoja na wale wa jumuia za watumia maji wa Wakala wa maji na Usafi wa Mazingira vijijji(RUWASA).

Amesema Serikali imetoa muongozo ili kuwawezesha wananchi kupata huduma ya maji safi na salama kwa bei nafuu.

“Serikali imekuja na utaratibu wa kutoza wananchi maji kila wanapokwenda kuchota maji, zamani jumuiya zilikuwa zikijipangia bei na bei hizi mpya zimeanza mwezi huu.”

Maji ambayo mashine yake inatumia dizeli, ndoo moja haipaswi kuzidi Sh50, kwa msukumo wa nguvu ya umeme ni sh 40 na maji yanayopatikana kwa umeme wa jua ni sh 30 na maji ya mserereko ndoo isizidi Sh 25,” amesmea

Aidha amezitahadharisha jumuiya ambazo huduma ya maji ilikua inapatikana kwa bei ya chini zaidi na ile ya muongozo kutotumia bei hizo kupandisha gharama kwa gafla na badala yake watoe huduma bora kwa gharama nafuu na inapotokea changamoto wapandishe bei kwa kutazama uhalisia wa kipato cha  wananchi wa eneo husika.

Katika hatua nyingine, Shigella amepiga marufuku tabia ya baadhi ya watumishi wanaopewa vifaa vya usafiri kuvitumia kwa malengo binafsi kwa kuwapa vijana kuzitumia kwenye biashara ya bodaboda na kujiingizia kipato kinyume na malengo yaliyokusudiwa.

“Wapo baadhi ya watumishi wanageuza pikipiki kuwa sehemu ya bodaboda kila siku waletewe Sh5000 au Sh10, 000 hii ni kinyume cha sheria na ukosefu wa maadili unalipwa mshahara unaweza kukopa benki na kufanya biashara yako nataka mkazitunze zilete tija iliyokusudiwa”alisema Shigella

Awali meneja wa Ruwasa mkoani hapa Jabir Kayilla amesema mahitaji ya maji vijijini kwenye mkoa huo ni lita 53.4 milioni lakini yanayozalishwa ni lita 36.3milioni hivyo kuwa na upungufu wa lita 17.1 milioni sawa na asilimia 32 kwa siku.

Mkoa huo wenye vijiji 487 vyenye huduma ya maji safi ni vijiji 353 na kusababisha wananchi wa vijiji 133 kukosa huduma ya mai safi na salama.

Amesema serikali imekua ikiendelea kupeleka huduma za maji kwa wananchi ambapo kwa mwaka 2021 miradi 16 ilitekelezwa pamoja na uchimbaji wa visima 36 na miradi hiyo ikikamilika itaongeza huduma ya maji kutoka asilimia 68 zilizopo sasa hadi kufikia asilimia 76 ifikapo disemba 2022.