Saa 72 za Dk Malasusa, milima na mabonde ya Askofu Shoo

Askofu Alex Malasusa

Muktasari:

  • Safari ya uongozi wa Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo inatamatika Januari 21, 2024 kwa nafasi yake ikichukuliwa na Askofu Alex Masasula. Miaka takribani tisa ya Askofu Shoo imekuwa na milima na mabonde.

Moshi. Saa za Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo kukalia kiti hicho zinahesabika na hazizidi saa 72 kutoka sasa atalazimika kumkabidhi kijiti mkuu wa kanisa hilo mpya, Askofu Alex Malasusa.

 Ni tukio linalovuta hisia za waumini wengi wa KKKT kwa kuwa takribani miaka tisa iliyopita, Askofu Malasusa ndiye aliyemwingiza kazini Askofu Shoo kama mkuu wa Kanisa, lakini Januari 21, 2024 Askofu Shoo anamkabidhi tena Askofu Malasusa.


Matangazo yanayosambaa katika mitandao ya kijamii ikiwamo makundi ya Whatsapp, yanaonyesha ibada ya kumuingiza kazini Askofu Malasusa kama mkuu mpya wa Kanisa, itafanyika Kanisa Kuu la Azania Front jijini Dar es Salaam.

Kwa kawaida, ibada kama hiyo huhudhuriwa pia na kiongozi kutoka serikalini, ingawa hadi sasa bado haijajulikana ni kiongozi gani hasa atakuwa mgeni rasmi, lakini pia huhudhuriwa na maaskofu wa KKKT na makanisa mengine marafiki, wachungaji na wamumini.

Askofu Malasusa ambaye kwa sasa ni mkuu wa Kanisa mteule na pia mkuu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, kuanzia leo Alhamisi Januari 18, 2023 hadi Januari 21 atakapoingizwa rasmi kazini, atakuwa na saa takribani 72 za kusubiri.

Uchaguzi huo wa Askofu Malasusa uliofanyika usiku wa Agosti 25, 2023 uliofanyika katika ukumbi wa chuo Kikuu cha Tumaini Makumira (Tuma) kilichopo Arusha, ulilazimika kurudiwa mara tatu baada ya mshindi kutopata theluthi mbili ya kura.

Mara ya kwanza kura zilizopigwa zilikuwa 253 ambapo Dk Malasusa alipata kura 90, Askofu Abednego Keshomshahara wa wa Dayosisi ya Kaskazini Magharibi kura 83 na Askofu George Fihavango wa Dayosisi ya Kusini (Njombe akipata kura 69.


Kwa mujibu wa Katiba ya KKKT, theluthi mbili ya kura haikupatikana ili kupata mshindi hivyo uchaguzi ukarudiwa kwa mara ya pili kwa wagombea wawili waliopata kura nyingi ambao ni Askofu Malasusa na Askofu Keshomshahara.

Hata hivyo, katika uchaguzi wa duru ya pili, theluthi mbili haikufikiwa ambapo Dk Malasusa alipata kura 142 na Keshomshahara kura 96 kati ya kura 239 zilizopigwa na hivyo uchaguzi kutangazwa kurudiwa kwa mara ya tatu.


Katika uchaguzi wa duru ya tatu, Askofu Malasusa alipata kura 167 sawa na asilimia 69.3 ya kura 241 zilizopigwa huku Keshomshahara akipata kura 73 sawa na asilimia 30.3 na hivyo Malasusa kutangazwa kuwa mkuu mteule wa kanisa hilo.

Uchaguzi wa Askofu Malasusa uliibua mijadala si kwa waumini wa KKKT pekee, bali kwa Watanzania kupitia mitandao ya kijamii wakihoji Malasusa akarudi tena kuwa mkuu wa Kanisa baada ya kuhudumu cheo hicho kati ya 2007 hadi 2015.

Hata hivyo, Katibu mkuu wa zamani wa KKKT kwa miaka 16 (1988-2005), Amani Mwenigoha alinukuliwa na gazeti la Mwananchi akisema Katiba ya KKKT haina ukomo wowote na kusema hata Askofu Shoo angeweza kuchaguliwa kipindi kingine.


Askofu Shoo na Milima, mabonde


Askofu Shoo ambaye pia ni mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT anaondoka akiwa ameliachia kanisa hilo Katiba moja, lakini akiwa amepita katika milima na mabonde katika uongozi wake hasa uchaguzi wa kipindi chake cha pili.

Katika mzunguko wa kwanza wa uchaguzi huo uliofanyika Agosti 2019, Askofu Shoo alipata kura 144 huku mpinzani wake, Askofu Keshamshahara akipata kura 74 kati ya kura 218 za wajumbe wa mkutano na kushindwa kupata theluthi mbili.

Kwa kuwa Askofu Shoo hakuwa amepata ushindi wa zaidi ya theluthi mbili, uchaguzi huo ulikuwa uingie mzunguko wa pili, lakini hata hivyo Askofu Keshamshahara akaondoa jina lake na hivyo Askofu Shoo kushinda uchaguzi huo.

Kwa sura ya kawaida, unawezekana ukaonekana ulikuwa uchaguzi wa kawaida wa kumpata mkuu wa kanisa, lakini kiuhalisia kulikuwa na nguvu zilizokuwa nje ya Katiba na Kanuni za Kanisa hilo kubwa nchini za kumpata Kiongozi huyo.


Hata hivyo, Shoo alifanikiwa kuvuka viunzi katika uchaguzi huo mgumu ndani ya KKKT ambao ulidaiwa kutaka kuligawa kanisa hilo katika makundi mawili.

Ugumu huo unatokana na ukweli kuwa kulikuwepo na nguvu nje ya zile za kawaida na kidemokrasia ambazo hutumika kumpata mkuu wa Kanisa anayeomba kupata ridhaa ya kipindi cha pili, akitarajiwa kubebwa na kazi alizozifanya.


Katiba moja ya KKKT


Moja kati ya mafanikio ambayo Askofu Shoo analiachia kanisa hilo ni mabadiliko ya kishindo ya Katiba yake ambapo wajumbe 214 kati ya 248 wa mkutano mkuu wa 21 wa KKKT, waliridhia pendekezo la Kanisa hilo kuwa na Katiba moja.

Kwa mabadiliko hayo, Katiba hiyo mpya inakwenda kuondoa Katiba za Dayosisi zake 27 ambazo zinazipa mamlaka kamili ya kujiendesha na sasa KKKT linakwenda kuwa na mkuu wa kanisa mwenye mamlaka makubwa zaidi kuliko hapo awali.

Kupitishwa kwa pendekezo hilo, mkuu wa kanisa atakuwa na uwezo wa kuwachukulia hatua maaskofu na wachungaji wanaokiuka maadili na hatafanya hivyo peke yake, bali kwa kutumia chombo cha kikatiba kitakachoundwa.


Muundo huu, unaelezwa kuwa na tiba iliyotafutwa kwa muda mrefu ya namna ya kushughulikia migogoro na nidhamu katika dayosisi kwa kuwa kwa Katiba ya sasa, kila dayosisi ina mamlaka kamili kisheria na ina vyombo vyake vya maamuzi.


Kwa mabadiliko hayo yanayokwenda kufanywa, inaelezwa kuwa dayosisi hizo zitaendelea kuwa na mkuu wa dayosisi, msaidizi wa askofu na vyombo vyake, lakini sasa vitaendeshwa kwa kutumia kanuni ndogo ndogo zitakazotungwa.


Waraka wa Pasaka


Katika moja ya mambo yaliyomtikisa Askofu Shoo na kanisa ni waraka wa Pasaka wa Machi 24 uliosainiwa na maaskofu 27 wa KKKT waliokutana Machi 15, 2018, waraka ambao ulisomwa katika sharika zote za dayosisi zote 27 nchini Machi 25.


Waraka huo uligusia mambo ambayo maaskofu walisema hayaendi sawa ikiwa ni pamoja na kuminywa kwa demokrasia na uhuru wa habari na kujieleza, kuminywa kwa utawala wa sheria na watu kupotea, kuuawa na kuokotwa kwenye viroba.

Uzito wa maudhui ya waraka huo, yalilifanya kanisa hilo kuingia katika msuguano na Serikali iliyokuwa ikiongozwa na Rais John Magufuli ambapo msajili wa taasisi za dini katika Wizara ya Mambo ya Ndani akaliandikia barua akilitaka kufuta waraka huo.

Barua ya Mei 30, 2018 aliyoandikiwa mwenyekiti au Askofu mkuu wa KKKT, ilitoa maelekezo ya kufutwa kwa waraka huo kwa maelezo kuwa ulikuwa umetolewa na chombo ambacho hakitambuliki kisheria na msajili wa taasisi hizo za dini.

“Unaelekezwa kuufuta waraka husika kwa maandishi na kuujulisha umma kuwa taasisi hiyo haikuwa na haina uwezo wa wa kisheria kufanya kile mlichokifanya”, ilisema barua hiyo iliyokuwa imetiwa saini na M.L Komba kwa niaba ya Msajili.