Saba kortini wakidaiwa kusafirisha sukari, mafuta ya kula kwa magendo

Muktasari:


  • Watu hao  wanakikabiliwa na mashtaka manne likiwemo la kusafirisha sukari na mafuta ya kula kwa njia ya magendo huku wakikwepa kulipa kodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA).

Dar es Salaam. Watu saba wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka manne likiwemo la kusafirisha sukari na mafuta kwa njia ya magendo yenye zaidi ya Sh 10.7 milioni.

 Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka kwa mahakimu watatu tofauti ambao ni Hakimu Mkazi Mwandamizi, Veneranda Kaseko, Hakimu Mkazi, Nabwike Mbaba na Ramadhani Rugemalira, leo Alhamisi, Machi 7, 2024.

Washtakiwa hao ambao ni wakazi wa Kunduchi, Dar es Salaam ni mfanyabiashara, Mustapha Bakari (30), dereva ni Mohamed Nassor (25) na Abdulmajid Kheri (17) na Erick Solomon Mwagemba (25), Justin Mollel (35).

Wengine ni wavuvi wawili ni Mbaraka Mwanjovu (23)  na Hamad  Hamad maarufu Katoto (23).

Wakili wa Serikali, Auni Chilamula akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Nabwike Mbaba amedai washtakiwa Nassoro na Kheri Februari 11, 2024 maeneo ya Kunduchi wilayani Kinondoni walikutwa wakiingiza mifuko 20 ya sukari kwa kutumia njia ya magendo hivyo kukwepa ushuru wa zaidi Sh2.3 milioni kinyume na sheria.

Chilamula amedai tarehe hiyo na mahali hapo washtakiwa hao walikwepa ushuru kwa kuingiza mifuko 20 ya sukari kwa kutumia gari T 956 BBF.

Pia amedai washtakiwa hao walishindwa kuwasilisha nyaraka za bidhaa pamoja na kukutwa na bidhaa za magendo.

Chilamula akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Kaseko, amedai mshtakiwa Erick anadaiwa kusafirisha mifuko 20 ya sukari kupitia bandari bubu na kukwepa ushuru wa Sh2.3 milioni.

Pia, akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Rugemalira, washtakiwa Mollel,  Mwanjovu na  Hamad wanadaiwa  Februari 11,2024 maeneo ya Mtongani - Kunduchi jijini Dar es Salaam walisafirisha madumu 100 ya mafuta ya kupikia kwa kupitia bandari bubu na kuisababisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya Sh4.02 milioni.

Kwa upande wa Bakari, anadaiwa Februari 11, 2024 maeneo ya Mtongani Kunduchi, wilayani Kinondoni kinyume na sheria aliingiza madumu 50 ya mafuta ya kupikia  kupitia bandari bubu na kusababisha ukwepaji wa kodi zaidi ya Sh2 milioni.

Katika shtaka la pili, inadaiwa tarehe hiyo na maeneo hayo Bakari akiwa dereva wa gari T 964 DPJ aina ya Toyota Bravis alisafirisha madumu 50 ya mafuta ya kupikia yaliyotoka nje ya Tanzania.

Katika shtaka lingine inadaiwa katika tarehe hiyo na mahali hapo, Bakari alishindwa kuandaa taarifa ya usafirishaji wa madumu 50 ya mafuta ya kupikia huku akijua kuwa hiyo ni bidhaa hazijalipiwa na kusababisha kukwepa kodi ya Sh2.01 milioni.

Katika shtaka la nne, inadaiwa Bakari akiwa msimamizi na dereva wa gari T 964 DPJ aina ya Toyota Bravis, kinyume na sheria alikutwa akisafirisha madumu 50 za mafuta ya kula yaliyokuwa yakitoka nje ya Tanzania, huku akifahamu ni bidhaa za magendo.

“Upelelezi bado haujakamilika na ninaiomba Mahakama hii ipange tarehe nyingine ya kutajwa," amedai Chilamula.

Baada ya kusomewa mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa kuwa mashtaka wanaokabiliwa nayo ni ya uhujumu uchumi. Kesi hizo ziimeahirishwa hadi Machi 21, 2024 zitakapotajwa.