Prime
Sababu wananchi kupeleka malalamiko kwa wanasiasa

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda akizungumza na wananchi wa Maswa mkoani Simiyu baada ya kupokelewa mkoani humo katika mwendelezo wa ziara yake ya mikoa 20. Picha na CCM
Dar es Salaam. Tabia ya Watanzania kufurika kwenye mikutano ya wanasiasa na kueleza kero zao kuliko kwenda kwenye vyombo vya sheria kupata haki, imeelezwa kusababishwa na mifumo isiyo rafiki na ya uhakika ya kuwapa majibu.
Hayo yameelezwa siku chache baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Eliezer Feleshi akizungumza kwenye maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini, Februari Mosi, 2024 kueleza wananchi wanakwenda katika mikutano ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda kueleza yaleyale yanayopelekwa kwenye vyombo vya utoaji haki.
“Nikifuatilia ziara ya yule Katibu wa Itikadi wa CCM (Paul Makonda), naona wananchi bado wanajisomba kwake kwa mafuriko na hivyo hivyo ukifuatilia nyumba za ibada wananchi wanajisomba vilevile huko.
“Kwa hiyo sasa hii mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan), tunaichukulia kama changamoto, pamoja na kusoma kwetu, pamoja na kupata nyenzo na maboresho tunayoendelea nayo, tujue wananchi watahitaji vilevile kupata wanachokusudia kukipata,” alisema.
Kutokana na changamoto hiyo, Jaji feleshi alisema wameweka mkakati wa kuanzisha vituo vya huduma wezeshi saa 24, ili mtu akipata tatizo afike kwenye kituo na kuelekezwa taratibu za kuchukua.
Si kwa Makonda tu, hata mikutano ya upinzani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na ya ACT-Wazalendo ambayo imekuwa ikifanyika, wananchi wamekuwa wanakwenda kutoa kero zao na viongozi wake wamekuwa wakiiitaka Serikali kuzishughulikia.
Haiishii hapo, hata ziara za viongozi waandamizi mathalani, Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na sasa Naibu Waziri Mkuu, wananchi wamekuwa wakienda na mabango ya kero zao.
Rais Samia Suluhu Hassan aliwahi kunukuliwa akisema viongozi wa kitaifa wakikutana na mabango katika ziara zao, atawaondoa kazini mkurugenzi wa halmashauri na wakuu wa wilaya husika.
Rais Samia alitoa kauli hiyo Aprili 6, 2021, Ikulu jijini Dar es Salaam, baada ya kuwaapisha makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu aliokuwa amewateua Aprili 4, 2021.
Alisema imekuwa ni kawaida viongozi wakifanya ziara mikoani na wilayani wanapokelewa na mabango ya wananchi wakilalamikia kero mbalimbali na masuala wanayolalamikia si ya kitaifa.
Pia Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma alizungumzia mifumo wa kidigitali iliyowekwa mahakamani pamoja na mfumo ya haki jinai, akisema haipaswi kukwaza utoaji haki.
Kauli za viongozi hao zimekuja wakati iliyokuwa Tume ya Haki Jinai imeshatoa mapendekezo yake ya kuboresha mfumo wa utoaji haki nchini.
Akizungumzia utekelezaji wa mapendekezo hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mary Makondo amesema Serikali imeshaanza kufanyia kazi.
“Tunaendelea kufanyia kazi mapendekezo hayo, kuna utekelezaji wa muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu,” amesema.
Akijadili suala hilo jana, Februari 3, 2024 mwanasheria Dk Onesmo Kyauke amesema mfumo wa Mahakama una urasimu mrefu unaowakatisha tamaa wananchi kupeleka malalamiko yao.
“Mahakama ni chombo kizuri cha kupata haki, lakini kuna urasimu, upende usipende.
“Kwanza wananchi wengi hawana uelewa wa jinsi Mahakama inavyofanya kazi, pili hawana uwezo wa kulipia mawakili wanaozijua sheria na tatu, mahakamani kuna urasimu mwingi, kama kuleta mashahidi na mengineyo.
“Ndio maana wananchi wakiona wanasiasa wanaona ni rahisi kueleza matatizo yao na yanajibiwa pale pale,” amesema.
Amegusia pia suala la rushwa, akidai kuwepo kwa mianya ya maofisa wa Mahakama kuhongwa na hivyo kuwapa nafasi wenye uwezo wa fedha kupindisha haki.
Maelezo hayo yameungwa mkono na Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Harold Sungusia akirejea kitabu cha Profesa Issa Shivji cha Ujamaa Hegemony, kinachoeleza maisha ya Watanganyika kabla ya uhuru.
“Kabla ya kupata uhuru, kulikuwa na mkuu wa wilaya ambaye wakati huo aliitwa District Officer (DO). Huyo alikuwa ni mtawala na hakimu kwa wakati mmoja, hivyo watu walipeleka malalamiko kwake na alitoa hukumu,” amesema.
Amesema baada ya kuanzishwa kwa chama cha TANU, wananchi walizoeshwa kupeleka malalamiko yao kwenye chama hicho na yalipatiwa ufumbuzi.
“Utamaduni huo umeendelezwa hata ilipokuja CCM, watu wamekuwa wakipeleka malalamiko kwa viongozi wa siasa kuliko mahakamani,” amesema.
Amesema ulipoanzishwa mfumo wa Mahakama, watu wengi hawakuwa wameuzoea na isitishe, una milolongo mingi hadi mtu apate haki yake.
“Mchakato wa mahakama kwanza unaonekana sio rafiki, kwa mfano utaambiwa uandike barua na ifuate utaratibu wao. Unaona majaji wamevaa majoho mekundu, yanatisha.
“Halafu lugha inayotumika ni Kiingereza, ni tofauti na kwa wanasiasa, uwe unajua kusoma na kuandika au hujui, unaeleza shida yako unajibiwa. Kwa sababu wananchi wanachotaka ni kusikilizwa,” amesema.
Akinukuu ibara ya 107A (1&2) inayoeleza Mahakama kama mamlaka ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano.
“Katika kutoa uamuzi wa mashauri ya madai na jinai kwa kuzingatia sheria… yaani, kutenda haki kwa wote bila ya kujali hali ya mtu kijamii au kiuchumi, kutochelewesha haki bila sababu ya kimsingi.
“Kutoa fidia ipasayo kwa watu wanaoathirika kutokana na makosa ya watu wengine, na kwa mujibu wa sheria mahususi iliyotungwa na Bunge; kukuza na kuendeleza usuluhishi baina ya wanaohusika katika migogoro,” amesema.
Hata hivyo, amesema kumekuwa na sheria zinazotungwa za kuongeza masharti ya mchakato wa kufungua kesi, ambazo mtu akikosea tu shtaka lake linafutwa.
“Tufuate mfano wa India ambako mtu anaweza tu kuandika barua ya kawaida na kesi yake ikakubalika,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga amesema wamekuwa wakipigania kufanyika kwa marekebisho ya sheria zikiwamo Sheria ya Dhamana, Sheria ya Ushahidi, Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ili kurahisisha utoaji haki.
“Hata kesi za madai zina mlolongo mrefu na hazina kikomo. Utakuta mtu anashinda kesi ya miaka 10, lakini hadi alipwe inachukua miaka 10 mingine,” amesema.
Akizungumzia suala la wanasiasa kupelekewa malalamiko, Henga amesema suala hilo linafahamika kama ‘Kangaroo courts’ ambazo ni mahakama zisizo rasmi na wala hazina utaratibu unaoeleweka.
“Watu wanakwenda kwa wanasiasa, kwa sababu mfumo wa Mahakama ni mgumu, leo utaambiwa kesi imeahirishwa jaji ni mgonjwa, kesho jaji amesafiri, mwezi ujao hayupo. Ni mlolongo mrefu,” amesema.