Sabaya ashinda rufaa ya pili

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai,Lengai OleĀ  Sabaya,akizungumza na mke wake (Jesca Nasari), kabla ya hukumu iliyokatwa na DPP dhidi yake na wenzake wawili. Picha na Janeth Mushi

Muktasari:

  • Akisoma uamuzi huo Naibu Msajili huyo, amesema kuwa uamuzi uliofanywa na Mahakama Kuu ya Arusha wa kuwaachia washtakiwa hao, kufuta mwenendo licha ya kuwa haikuwa sahihi, lakini pia makosa ya unyang'anyi wa kutumia silaha ambayo yalibadilishwa na kufanywa unyang'anyi wa kikundi kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha pia hayakuthibitishwa.

Arusha. Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya ameshinda rufaa iliyokuwa imefunguliwa na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) dhidi yake na wenzake wawili.

Uamuzi huo umesomwa leo Ijumaa Novemba 17, 2023 na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa nchini, Abeesiza Kalegeya.

Hukumu hiyo iliyotolewa na Majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa wakiongozwa na Jaji Jacobs Mwambegele, Ignas Kitusi na Leiya Mgonya, waliosikiliza rufaa hiyo kwenye kikao chao kilichofanyika Arusha.

Akisoma uamuzi huo Naibu Msajili huyo, amesema kuwa uamuzi uliofanywa na Mahakama Kuu ya Arusha wa kuwaachia washtakiwa hao, kufuta mwenendo licha ya kuwa haikuwa sahihi, lakini pia makosa ya unyang'anyi wa kutumia silaha ambayo yalibadilishwa na kufanywa unyang'anyi wa kikundi kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha pia hayakuthibitishwa.

Mahakama hiyo imemuachia huru Sabaya ambaye alikuwa mahakamani hapo huku wajibu rufaa wenzake Sylvester Nyegu na Daniel Mbura, ambao hawakuwa mahakamani hapo.

Hii ni rufaa ya pili Sabaya na wenzake kushinda, ambapo awali Mei 6, 2022, Mahakama Kuu Kanda ya Arusha iliwaachia huru na kukubaliana na rufaa yao.

Awali Oktoba 15, 2021 Hakimu Mkazi Mwandamizi, Odira Amworo, aliwahukumu Sabaya na wenzake kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya unyang'anyi wa makundi kwani Jamhuri ilishindwa kuthibitisha makosa ya unyang'anyi wa kutumia silaha waliyokuwa wameshitakiwa nayo awali.

Baada ya kutoka mahakamani hapo, baadhi ya watu waliokuwepo mahakamani hapo wakiwemo viongozi wa dini, ndugu na jamaa walimfanya maombi ya pamoja na shukrani.

Akizungumza nje ya mahakama, Sabaya amesema Mungu ametenda haki.