Sakata Tanga Cement lamuibua Jaji Mihayo

Dar es Salaam. Sakata la ununuzi wa Kampuni ya Tanga Cement limeendelea kugonga vichwa vya wadau wa sheria na sasa ni zamu ya Jaji mstaafu Thomas Mihayo anayesema Serikali inapaswa kuheshimu na kutekeleza uamuzi wa Mahakama.
Jaji Mihayo anasema Taifa lolote lisiloheshimu uamuzi wa Mahakama ni hatari kwa kuwa linaweza kuwakimbiza wawekezaji wakijua lina tabia hiyo.
“Ninachofahamu, kitu ambacho sisi majaji kinatukera na mimi kinanikera ni kutafuta njia ya kutokutii amri ya Mahakama, ni jambo ambalo ni hatari kwa Taifa,” alisema Jaji Mihayo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Majaji Wastaafu Tanzania.
Alichokizungumza Jaji Mihayo ni uamuzi wa Baraza ya Ushindani (FCT) uliositisha mchakato wa ununuzi wa Kiwanda cha Saruji Tanga huku akisema kama Serikali inaona mazingira yamebadilika inapaswa kurudi kwenye Mahakama kuomba marejeo na si vinginevyo.
Ununuzi wa kiwanda hicho licha ya kupatiwa baraka za Tume ya Ushindani (FCC) Oktoba 2021 kwa gharama ya Sh137 bilioni, Septemba 2022, FCT ilibatilisha baraka hizo.
Uamuzi wa FCC ungeipa kampuni ya Scancem International DA (Scancem) – kampuni tanzu ya Heidelberg Cement AG, inayomiliki Twiga Cement, uwezo wa kununua asilimia 68.33 ya hisa za Tanga Cement baada ya kukubaliana na Kampuni ya Afrisam.
Anachokieleza Jaji Mihayo kimewahi kuzungumzwa Aprili 10 mwaka huu na aliyekuwa Rais Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Profesa Edward Hoseah, aliyeipongeza FCT kwa kusitisha mchakato wa ununuzi wa kiwanda hicho.
Profesa Hoseah ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), alisema uamuzi wa Septemba 23, 2022 wa FCT, “lazima uheshimiwe kwa kuwa ulionyesha wazi uhitaji wa kuwalinda watumiaji wa huduma.”
Jana, Jaji Mihayo akichangia maoni yake juu ya sakata hilo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, alisema wanachokizungumza mawaziri kwamba mazingira ya wakati huo na sasa yamebadilika, hayaathiri uamuzi wa Mahakama.
“Kwa hiyo haijalishi mazingira yamebadilika, Mahakama imezuia muungano wowote moja kwa moja wa aina yoyote,” alisema Jaji Mihayo
Alisema, “nafahamu uamuzi wa hii Mahakama ni wa mwisho. Kama hujaridhika unaomba mapitio, mimi ninavyoona mawaziri hawakushauriwa vizuri katika suala hili.”
Alipoulizwa ikiwa uamuzi huo wa Mahakama utapuuzwa na muungano kuendelea, Jaji Mihayo alisema, “mimi siwezi kuangalia kinachoendelea sasa, lakini ukiangalia uamuzi wa Mahakama ulizuia na kama kuna mtu anataka kuendelea anapaswa kurudi mahakamani.”
Jaji Mihayo alisema wizara kama inataka muungano wa kampuni hizo mbili, “ingerudi mahakamani kuomba marejeo.”
Katika hilo, Jaji Mihayo alisema, “yaani ni kwamba mfano Mahakama iseme Mihayo na Zena wasioane, hawawezi kuoana.”
Alitahadharisha kinachoendelea kwa kupuuzwa kwa uamuzi wa Mahakama akisema, kwa sasa kampuni duniani zinatembea, “wakiona kama uamuzi wa Mahakama unaweza kupuuzwa, wanaogopa kuingia.
“Nia njema ya Rais kuvutia wawekezaji wanaweza kuivuruga. Kampuni yoyote ikiona kwa ngavu ya mawaziri wanaweza kutoa kauli zile ni hatari,” alisema.
Sakata hilo liliibua mjadala mkubwa ndani na nje ya Bunge, wengine wakipinga kwa madai kuwa itasababisha ukiritimba kwenye soko, huku wengine wakisema kuzuia muunganiko huo ni kwenda kinyume na masuala ya biashara.
Mjadala huo ulipamba moto zaidi wakati wa bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mei 4 na 5 mwaka huu na kuwalazimu mawaziri watatu, Dk Ashatu Kijaji wa viwanda, Dk Mwigulu Nchembe wa Fedha na Mipango na Patrobas Katambi, naibu waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu kutoa ufafanuzi kuwa uwekezaji huo umefuata sheria.
Katambi alisema alithibitisha kinahesabu kwamba Kampuni ya Saruji ya Tanga haiwezi kujiendesha tena na kujikuta inashindwa kulipa kodi.
Alisema katika kipindi cha mwaka 2020 uamuzi uliyofanywa na FCT ulijikita zaidi kwenye tafiti zilizofanyika mwaka huo na kwamba kampuni ya saruji iliyokuwa inaongoza kwa mapato wlikuwa Twiga, Tanga na Dangote.
Sakata la Kampuni ya Tanga Cement lilianza Oktoba 2021, wakati Scancem International DA (Scancem) – kampuni tanzu ya Heidelberg Cement AG, inayomiliki Twiga Cement – na AfriSam Mauritius Investment Holdings Limited, mmiliki wa Tanga Cement, ilipotoa taarifa ya pamoja kuwa zimekamilisha masharti ya kupata asilimia 68.33 ya hisa katika kampuni ya Saruji Tanga.