Samia atoa pongezi mama anayekumbatia watoto Amana
Muktasari:
- Siku mbili baada ya gazeti na mitandao ya kijamii ya Mwananchi kutoa habari inayomhusu mama anayejitolea kutunza watoto njiti waliotelekezwa Hospitali ya Amana, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pongezi na kumtunuku Sh2 milioni.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pongezi kwa Mariam Mwakabungu (25), anayejitolea kukumbatia watoto njiti waliotelekezwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana.
Ujumbe huu umetumwa siku mbili tangu gazeti la Mwananchi na mitandao yake Jumapili Julai 16 kuripoti habari kuhusu Mariam na namna alivyosaidia watoto watatu waliotelekezwa na mama zao.
Samia ametuma ujumbe huo leo Jumatano, Julai 19, 2023 uliwasilishwa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Brayson Kiwelu ambaye amemkabidhi Mariam kiasi cha Sh2 milioni.
Dk Kiwelu amesema ujumbe huo umetumwa na Rais Samia ambaye amekuwa mstari wa mbele katika huduma za mama na mtoto.
"Rais ametoa Sh2 milioni fedha taslim kumpatia mama huyu kwa kujitoa kwake na amewapongeza viongozi wa Wizara ya Afya na Amana kwa ubunifu huu na uthubutu mama huyu kuwa sehemu yetu,” amesema Dk Kiwelu na kuongeza;
"Rais ameshukuru sana msaada ambao mama huyu ameutoa na amewataka Watanzania kuendelea kujitoa kwa ajili ya kuhudumia wale wenye uhitaji."