Serikali kuajiri wahudumu ngazi ya jamii 15,000

Muktasari:

  • Wakati Mawaziri wa Afya wa nchi tano ikiwemo Tanzania, Rwanda, Sierra Leon, Ethiopia na Jamhuri ya Afrika ya Kati wakikutana na kuweka mkakati wa kuanza kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii, Serikali ya Tanzania imesema tayari imeandaa muundo wa utumushi unaoitambua kada hiyo.

Kigali, Rwanda. Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Tanzania tayari inayo muundo wa utumishi (Scheme of Service) unaoitambua kada ya wahudumu wa afya ngazi ya jamii na kwamba inatarajia kuajiri watumishi 15,000 kwa kipindi cha miaka mitatu 2023/2026.

Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazroui akifurahia jambo na mtoa huduma wa kliniki ya chanjo kwa njia ya simu inayotembea iliyopo Kigali Rwanda. Kuanzishwa kwa kliniki hiyo ni sehemu ya juhudi za kukuza upatikanaji wa chanjo na huduma nyingine za afya kwa jamii ambazo hazijafikiwa barani Afrika.

Ummy ameyasema hayo kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Mawaziri wa Afya wa Afrika unaofanyika Jijini Kigali-Rwanda, unaojadili mifumo endelevu na stahimilivu ya uimarishaji wa huduma za afya ikiwemo masuala ya kuwatumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii.

Amesema watumishi hao wataajiriwa katika kutekeleza majukumu yao kama wasaidizi wa afya (Health Assistants) ngazi ya vituo vya kutolea huduma za afya na katika ngazi ya jamii.
Waziri Ummy amesema Tanzania ina uzoefu wa kuendesha mafunzo ya mwaka mmoja kwa kada rasmi ya wahudumu wa afya ngazi ya jamii ambapo zaidi ya wahudumu 9,800 walihitimu mafunzo hayo kwa mwaka 2017 hadi 2019.

“Wizara yangu itajikita katika kutekeleza mpango huu kwa kuwajengea uwezo na kuwaajiri wahudumu 15,000 kwa kipindi cha miaka mitatu yaani mwaka 2023/24 hadi 2025/26 ambapo kwa kuanzia wahudumu wapatao 5,000 watapewa mafunzo kupitia vyuo vya afya vya kati kwa mwaka wa fedha 2023/24,” amesema Waziri Ummy.

Amesema wahudumu hao watatekeleza afua jumuishi ikiwemo afya ya mama na mtoto, lishe, magonjwa yasiyoambukiza, magonjwa ya mlipuko na magonjwa yanayoambukiza (VVU/Ukimwi, kifua kikuu na malaria).

Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Nassor Mazrui amesema wizara yake inatarajia kuwatumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii katika utekelezaji wa huduma za kipaumbele ikiwemo magonjwa yasiyoambukiza, magonjwa ya mlipuko na afya ya mama na mtoto kwa ngazi ya shehia zote visiwani Zanzibar.