Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali kuajiri watumishi wapya 23,000

Muktasari:

  • Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), imesema imepokea kibali cha ajira mpya za walimu na maofisa afya.

Dar es Salaam. Serikali imesema itatoa ajira mpya za walimu na maofisa afya 23,000 katika kipindi cha Januari hadi Februari, mwaka huu.

 Waziri wa  Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa, amesema hayo leo Jumamosi, Januari 6, 2024 alipofunga kikao kazi cha makatibu tawala wasaidizi elimu na maofisa elimu wa halmashauri kilichofanyika mkoani Morogoro.

Amesema baada ya ajira 13,000 zilizotolewa kwa walimu walioajiriwa na kupangiwa maeneo, Serikali inaongeza nyingine mpya.

“Katika kipindi hiki cha Januari na Februari tayari Tamisemi tuna kibali cha ajira za walimu na hivi karibuni tutatangaza, ni pamoja na maofisa afya. Jumla watakuwa 23,000 wataajiriwa hivi karibuni,” amesema.

Mchengerwa amesema hatua hiyo inatokana na kuongezwa shule mpya 302 na madarasa 1,668 yatakayopokea wanafunzi Januari 8, 2024.

Amesema hayo ni maandalizi ya miradi ambayo imekuwa ikifanywa na Serikali, ikiwamo ya kuongeza shule na madarasa kupitia mradi wa kuimarisha na kuboresha elimu ya awali na msingi (Boost).

“Serikali imepanga kutumia Sh1.15 trilioni kupitia mradi wa Boost kuboresha miundombinu ya elimu ya awali na msingi, zimepangwa kutumika katika kipindi cha miaka mitano.  Tunakusudia kujenga madarasa 12,000 na vyoo 6,000 ifikapo mwaka 2025 kupitia mradi huo alioubuni Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema.

Amesema Sh1.2 trilioni zimetumika kwa shule za sekondari, zikiwamo mpya 1,000 za kata na 26 za wasichana za mikoa zilizojengwa na zitapokea wanafunzi Januari 2024.

Mchengerwa amesema katika kuhakikisha mtoto wa Tanzania anapata elimu bure, Serikali imekuwa ikitumia takribani Sh33.3 bilioni kila mwezi katika ufadhili wa elimu bila ada.

Amesema ili kuhakikisha elimu inafanikiwa, Serikali imeboresha mazingira ya walimu kwa kuwapandisha madaraja 227,263 na kuwalipa wanaodai malimbikizo.

Mchengerwa amewaagiza maofisa hao kuhakikisha wanaondoa kero za walimu ili kuboresha mazingira yao na kuwataka kupunguza malalamiko ya kada hiyo.

“Sitaki kusikia malalamiko ya walimu kama ambavyo nilifanya nikiwa Utumishi, kulikuwa na maofisa walifanya kusudi takribani 58 niliwavua vyeo. Nilifanya maamuzi magumu nikiwa Utumishi. Sitaki walimu wanyanyasike, heri niwafurahishe walio wengi kuliko wachache,” amesema na kuongeza:

“Kusimamia masilahi ya walimu nitafanya maamuzi magumu; kuonea, kunyanyasa na kuficha mafaili ili wasipandishwe vyeo sitasita kuchukua hatua.”

Mchengerwa amewataka watumishi hao, walimu na wengine wote walio chini ya Tamisemi kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii.

Amesema asilimia 76 ya watumishi wa umma wapo ndani ya Tamisemi ambayo ipo katika kila mkoa, wilaya, kijiji na kitongoji, hivyo wana wajibu wa kufanya vizuri.

“Msingi wa kufanya vizuri Tamisemi ni wa lazima, nadhani hiyo lugha imeeleweka vizuri na simbembelezi mtu na hasa wasaidizi wangu ni lazima,” amesema na kuongeza:

 “Tamisemi ndiyo injini ya Serikali, hii ndiyo injini ya nchi, wizara ya wananchi hii ndiyo nguzo ya Taifa letu. Tukifanya vizuri Tamisemi wizara zingine zote zitafanya vizuri na msingi wa wizara zote unategemea Tamisemi.Nawaambia wazi kabisa na yule atakayeona yeye anajivutavuta sitasita kumchukulia hatua. Hili nimelisema na nitaendelea kulirudia, kila mmoja lazima afanye kazi kwa bidii hakuna kubembelezana.’’

Aidha, Mchengerwa amewaagiza makatibu tawala na maofisa elimu kuhakikisha maboma ambayo yalitakiwa kukamilika mwaka 2023 yakamilike ifikapo Januari 15,2024.

“Niwaombe nendeni mkasimamie miradi hii, hasa katika maeneo yasiyo na visingizio. Fedha mlipokea kwa wakati, nendeni mkasukume gurudumu hili kabla ya tarehe tajwa na hili nimewaagiza wakuu wa mikoa na wameniahidi,” amesema.

Amewataka kuhakikisha shule zote zilizokamilika kwa asilimia 70 zisajiliwe na kuanza kupokea wanafunzi.

Awali, Naibu Katibu Mkuu, Tamisemi (Elimu), Dk Charles Msonde amesema idadi ya watoto wanaomaliza darasa la kwanza wanaojua kusoma na kuandika kwa mwaka 2022 imeongezeka kufikia asilimia 94.4 kutoka asilimia 61.

Amesema kwa ambao waliingia darasa la pili mwaka 2022, idadi pia imeongezeka na kufikia asilimia 95.

Dk Msonde amesema kazi kubwa inapaswa kufanyika katika stadi za kufundisha kwa walimu wa shule za sekondari, kwa kuwa kidato cha kwanza wanaoanza muhula Januari 8,2024 waliofaulu lugha ya Kiingereza ni asilimia 34.

“Asilimia 34 ndiyo waliofaulu somo la Kiingereza, hivyo watakuwa na kazi kubwa ya kujifunza kwanza lugha ndipo waweze kujua Kiingereza,” amesema na kuongeza:

“Wale wa kidato cha kwanza wa mwaka jana walimu wa sekondari wamefanya kazi kubwa, ambao kwa sasa watakuwa kidato cha pili. Maelekezo yako ndiyo yaliyoleta matokeo haya leo hii watoto wa darasa la tatu tunahakikisha wanaanza kuifahamu lugha,” amesema.

Akizungumzia tathmini ya hali ya chakula, amesema asilimia 66 ya shule za msingi zimeanza kutoa chakula kutoka asilimia 50 ya awali.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amesema kwa mwaka 2024, mkoa huo unatarajia kusajili wanafunzi 84,600 wa darasa la kwanza.

Amesema idadi hiyo itahitaji madarasa 2,638 na madawati 39,000, hivyo kuna upungufu wa madarasa 1,100 na madawati 10,200.