Serikali kuja na vigezo vipya madereva mabasi ya shule

Muktasari:

  • Aprili 12 mwaka huu wanafunzi wanane na msamaria mwema aliyejitosa kuwaokoa walifariki dunia baada ya gari walilokuwamo kusombwa na maji

Dar es Salaam. Kufuatia matukio kadhaa yaliyotokea ya magari ya kubeba wanafunzi, Serikali ya Tanzania inakusudia kuja na vigezo vipya vya madereva wanaoendesha mabasi ya shule.

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo amesema wizara walitoa mwongozo wa mabasi ya shule na kwamba waliviachia vyombo vingine vya Serikali kuendelea na ukaguzi wa madereva hao kama wanavyofanya kwa madereva wengine na hawakuwahi kuwa na mfumo.

“Baada ya uzoefu huu tutatafakari, namna gani nzuri tutaangalia dereva yupi atafaa kubeba watoto ni suala ambalo sasa tulifikirie kwa umbali zaidi kama Serikali tunapaswa kufanya nini katika suala hili.

“Katika mifumo ya kiserikai tayari dereva awe amekidhi vigezo lakini sasa utahitajika ukaguzi zaidi kwa madereva wa watoto, kulitafakari kwa pamoja na vyombo vingine na kulitolea msimamo. Kama kutakua na uhitaji wa kuongeza sifa za ziada kupitia mifumo ya serikali,” amesema Profesa Nombo.

Mtendaji mkuu huyo wa wizara amesema hayo leo Jumapili, Aprili 14, 2024 alipozungumza na Mwananchi Digital lililotaka kujua hatua ambazo Serikali inakusudia kuchukua kutokana na uwepo wa ajali zinazohusisha mabasi ya wanafunzi.

Miongoni mwa ajali hizo ambazo inadaiwa imesababishwa na uzembe wa dereva ni ya gari Toyota Hiace la Shule ya Msingi Ghati Memorial, kuangukia kwenye korongo lililojaa maji eneo la Dampo mkoani Arusha.

Wanafunzi wanane na msamaria mwema aliyejitosa kuwaokoa walifariki dunia. Ni tukio lililotokea asubuhi ya Aprili 12, 2024. Miili yao imeagwa leo Jumapili.

Katika maelezo yake, Profesa Nombo amesisitiza ili dereva aweze kukabidhiwa gari la wanafunzi lazima awe na vigezo na kazi ya trafiki ni kuwakagua kama wana vigezo na kupitia mchakato wa kuwa dereva.

“Madereva wanaobeba watoto wa shule, wanapaswa wawe makini zaidi tunategemea aliyekabidhiwa jukumu hilo, atazingatia kulinda uhai wa wale anaowabeba,” amesema.


Mwongozo

Waraka wa Elimu Na. 01 wa mwaka 2023 kuhusu uboreshaji wa huduma ya magari au mabasi yanayotumika kusafirisha wanafunzi, ulioanza kutumika Machi Mosi 2023 ulielekeza umakini kwa wamiliki wa shule kwa kuwa kuwa thamani ya rasilimali watoto ni kubwa kuliko thamani ya rasilimali yoyote ambayo nchi imejaliwa kuwa nayo.

Waraka huo uliolenga kuboresha utoaji wa huduma ya usafiri wa magari na mabasi kwa wanafrunzi uliwataka kuzingatia kutokuwepo kwa viashiria vyovyote vya ukatili dhidi ya wanafunzi ikiwemo ubakaji na ulawiti na tabia zenye viashiria vya mmomonyoko wa maadili.

“Tabia hizi zinaleta mmomonyoko wa maadili, kuathiri ukuaji, ujifunzaji na kuhatarisha ustawi wa watoto kwa ujumla. Haitakiwi kuwa na wahudumu jinsi moja ya wanaume pekee, kuweka miziki au nyimbo au picha za video zisizozingatia maadili, mila na destrui na tamaduni, kuwafanyia vitendo vya ukatili,” ulielekeza.

Mwongozo huo uliosainiwa na Kamishna wa Elimu, Dk Lyabwene Mtahabwa ulielekeza shule kuwa na ratiba rafiki za safari ili wanafunzi hususani watoto wadogo wapate muda wa kutosha kupumzika kwa ajili ya ukuaji wao.

Pia, uliekeza kuwa na mabasi yenye vioo angavu, wamiliki kuhakikisha wanaowaajiri wawe waaminifu, wenye weledi na maadili.

“Endapo mhudumu yeyote ataenda kinyuma na maadili au kuhatarisha usalama wa wanafunzi, mmiliki wa shule achukue hatua mara moja dhidi ya mtumishi husika.”

Maoni ya wadau

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chama cha Mabasi Tanzania, Majura Kafumu amesema sekta binafsi imetupwa kila mmiliki wa shule anachagua kipi kinachomfaa na ndiyo chanzo cha kuwa na maredeva wazembe.

Amesema iwapo Serikali ingethamini, anataja udereva ni sekta nyeti inabidi iangaliwe kwa makini na si kuanza kutafuta nini kifanyike baada ya majanga.

“Kwa nini tunafanya majaribio kwa watu walio hai? Si mabasi ya shule wala makubwa hata daladala bado ni tatizo hii sekta binafsi ingetambuliwa kisheria na Serikali wahudumu katika hiyo sekta wapatikane vipi na wathaminiwe vipi haya yasingejitokeza na ajali zingepungua,” amesema.

Kafumu ametaja changamoto iliyopo kwenye magari ya shule ni kutozingatia vigezo vya dereva bali huangalia unafuu wa ujira.

“Tunaacha mmiliki aelewane na dereva ni kitu kigumu kuelewana masikini na tajiri, lazima atachukua rahisi na siyo anayejielewa mwenye uzoefu wa miaka 20, ataona bora amchukue mtoto asiye na majukumu hata laki moja ataona inamfaa, anayejua majukumu anatambua umuhimu wa maisha,” amesema Kafumu.

“Ukimchukua aliyevuka miaka 35 tayari ana watoto nyumbani, ni mtu mzima ana familia bado baba na mama wanamtegemea, atasimamia majukumu yake anapokuwa kazini ili aweze kukidhi mahitaji yake.”

Mhandisi wa Magari na Mkuu wa Idara Msaidizi wa Idara ya Usafiri Salama na Mazingira Chuo cha Usafirishaji (NIT), Mhandisi Patrick Makule amesema kwa sasa wameanza kutoa mafunzo kwa madereva wa mabasi ya shule na mabasi ya kawaida kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini 9Latra).

Amesema mafunzo hayo yamekuja baada ya kujiridhisha huduma inayotolewa na madereva kwa wateja haikidhi.

Mhandisi Makule amesema kuanzia dereva mpaka matroni anayewahudumia watoto wote wanatakiwa kuwa na weledi na kuzingatia usalama wa watoto.

“Kuna mengi bado hawajayafahamu. Kuanzia usalama wao wakiwa kwenye gari, uangalizi wa watoto, wanapovuka maeneo hatari kama kwenye maji, watoto wanahitaji kulindwa na siyo kila mtu anaweza kuwa dereva ni wenye weledi, mafunzo maalumu pia. Serikali ipo kwenye hatua za mwisho kuhakikisha wote wanapata mafunzo,” amesema.


Ajali mabasi ya shule

Februari 27, 2024, basi la Shule ya Mchepuo wa Kiingereza ya New Vision ya jijini Arusha ilipata ajali na kusababisha vifo vya watu 11 wakiwemo raia wa kigeni.

Machi 24, 2024, eneo la Kata ya Kimwani wilayani Muleba mkoani Kagera, mwanafunzi mmoja wa Shule ya Sekondari ya Kemobos alifariki na wengine sita kujeruhiwa wakati wanafunzi 35 wa shule hiyo walipokuwa wakisafirishwa kwenda Kata ya Katoro wilayani Chato Mkoa wa Geita kwenda mapumzikoni (likizo).

Julai 26,2022, jumla ya wanafunzi wanane na watu wawili wa Shule ya Msingi, King David iliyopo mjini Mtwara walifariki dunia baada ya basi la shule walilokuwa wamepanda kutumbukia shimoni.

Mei 6, 2017 wanafunzi 32 wa Shule ya St Lucky Vincent, walimu wawili na dereva mmoja walifariki dunia kwa ajali ya gari.

Wanafunzi na walimu hao walikuwa safarini kuelekea Karatu kwenye Shule ya Tumaini English Medium Junior kufanya mtihani wa kanda wa majaribio ya kujipima uwezo kabla ya kufanya mtihani wa Taifa wa darasa la saba