Serikali kusaka fedha ujenzi bonde la Ruhuhu

Muktasari:

  • Serikali imesema upembuzi yakinifu uliofanyika mwaka 2013/14 ulibaini uwezekano wa kujenga bwawa kwa matumizi mbalimbali katika bonde la Ruhuhu ikiwemo kilimo cha umwagiliaji.

Dodoma. Serikali imesema upembuzi yakinifu uliofanyika mwaka 2013/14 ulibaini uwezekano wa kujenga bwawa kwa matumizi mbalimbali katika bonde la Ruhuhu ikiwemo kilimo cha umwagiliaji.

Hayo yamebainishwa na naibu Waziri wa Kilimo,  Hussein Bashe bungeni mjini Dodoma leo Jumanne Juni 8, 2021 na kubainisha kuwa katika bonde hilo wanaweza kuzalisha umeme wa megawati 300 wakati kilimo cha umwagiliaji kitakuwa ni hekta 4000.

Bashe alikuwa akijibu swali la mbunge wa Nyasa (CCM),  Stella Manyanya aliyetaka kujua mpango wa Serikali kuhakikisha bonde la Mto Ruhuhu lililopo kata ya Lituhi linawanufaisha wananchi kwa kuweka miundombinu ya kilimo na umwagiliaji.

Mbunge wa Nzega Mjini amesema  Serikali inatambua umuhimu wa bonde hilo linalojumuisha sehemu ya Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe na Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma linalotumika kwa kilimo cha umwagiliaji.

Amesema Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) linaendelea na upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa bwawa la Kikonge lililopo ndani ya bonde la mto Ruhuhu.

Bashe amesema mara baada ya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu itakapokamilika, Serikali itatafuta fedha za ujenzi wa bwawa hilo na

miundombinu ya umwagiliaji chini ya bwawa la Kikonge ili kuongeza uzalishaji na tija ya mazao ya kilimo katika eneo hilo.