Serikali: Utaratibu ulifuatwa kuhamisha wananchi Ngorongoro
Muktasari:
- Serikali imesema shughuli ya kuwahamisha wananchi kutoka Hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha kwenye kijiji cha Msomera wilayani Handeni Mkoa wa Tanga ulifuata taratibu na kulinda haki za binadamu.
Dodoma. Serikali imesema shughuli ya kuwahamisha wananchi kutoka Hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha kwenye kijiji cha Msomera wilayani Handeni Mkoa wa Tanga ulifuata taratibu na kulinda haki za binadamu.
Ufafanuzi huo umetolewa baada ya baadhi ya asasi za kiraia kusema haki za binadamu hazikuzingatiwa katika kuwahamisha wananchi hao.
Kauli hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki jijini Dodoma na baadhi ya mawaziri katika kikao kilichowakutanisha na timu ya wataalamu kutoka kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu ikiongozwa na kamishna wake, Dk Litha Ogana.
Wataalamu hao waliokuja nchini kufuatilia kuhama kwa wananchi wa Ngorongoro ambapo kabla ya kufanyika kwa mazungumzo hayo, kamisheni hiyo ilipata fursa ya kutembelea na kufanya mazungumzo na wananchi wa Ngorongoro na Msomera.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana ameieleza kamisheni kuwa shughuli ya kuwahamisha wananchi imefuata haki za binadamu kwani lilikuwa shirikishi na kwamba bado wananchi wanaendelea kujiandikisha kwa hiari.
‘’Serikali iliamua kufanya uamuzi kwa kuwa wananchi wa Ngorongoro walikuwa hawawezi kumiliki ardhi, kujenga makazi bora ya kudumu na kufanya mambo yao ya maendeleo kwa ajili ya mustakabali wa familia zao,’’ amesema Dk Pindi.
Aliieleza timu hiyo kuwa wanaoishi Ngorongoro wamekuwa wakikumbana na kadhia nyingi ambapo katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2020, watu 50 waliuawa na wanyamapori huku 148 wakijeruhiwa.
‘’Waliohamia Kijiji cha Msomera wamelipwa fidia, wamejengewa nyumba zenye staha pamoja na kupewa hati ya kumiliki ardhi, kupatiwa huduma zote za kijamii ambazo walipokuwa Ngorongoro walizikosa.’’
”…, wamelipwa fidia inayostahili pamoja na kusafirishiwa mizigo, mali na mifugo yao kuelekea kwenye makazi mapya na huu ndio msingi wa haki za binadamu.”
Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro amesema sheria zilizopo Tanzania hakuna kabila lolote linalomiliki ardhi ya mababu zao hivyo madai ya kwamba Wamasai wanatolewa kwenye ardhi ya mababu zao halina msingi wowote.
Naye kamishna wa kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu, Dk Litha Ogana amesema wamejiridhisha kuwa haki imetendeka katika kuwahamisha wakazi wa Ngorongoro na hakukuwa na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Shughuli ya kuhamisha wananchi wa tarafa ya Ngorongoro waliojiandikisha kuhama kwa hiari kwenda Kijiji cha Msomera ilianza Juni, 2022 na hadi Januari, 2023, kaya 523 zenye watu 2,808 na mifugo 14,757 zilikuwa zimeshahamia Kijiji cha Msomera na maeneo mengine.