Serikali ya Tanzania yaeleza ukuaji uchumi katikati ya corona

Serikali ya Tanzania yaeleza ukuaji uchumi katikati ya corona

Muktasari:

  • Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema licha ya mlipuko wa ugonjwa wa Covid 19, Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani zilizokuwa na ukuaji wa uchumi chanya.

Dar es Salaam. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema licha ya mlipuko wa ugonjwa wa Covid 19, Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani zilizokuwa na ukuaji wa uchumi chanya.

Amesema Pato la taifa la Tanzania lilikuwa kwa asilimia 4.8 ukilinganishwa na ukuaji wa asilimia 7.0 wa mwaka 2019.

Nchemba ameeleza hayo wakati akiwasilisha bungeni hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2020/21  na mpango wa maendeleo ya Taifa kwa mwaka wa fedha 2021/22 jijini Dodoma leo Alhamisi Juni 10, 2021.

Amebainisha kuwa sekta zilizochangia kwa kiwango kikubwa ukuaji wa juu wa mwaka 2020 ni pamoja na sekta ya ujenzi ambayo ilikuwa kwa asilimia 9.1, habari na mawasiliano asilimia 8.4, uchukuzi na uhifadhi wa mizigo 8.4, huduma zinazohusiana na utawala 7.8, shughuli za kitaalam 7.3, madini na mawe 6.7, afya na huduma za jamii 6.5.

“Wastani wa pato kwa mtu lilikadiriwa kufika shilingi milioni 2.6 sawa na dola za kimarekani 1151 kwa mwaka 2020 ikilinganishwa na shilingi za Kitanzania milioni 2.5 sawa na dola za Marekani 1118.9 kwa mwaka 2019 ikiwa ni ongezeko la asilimia 3.1,” amesema.