Serikali yaja na mwarobaini bei ndogo kwa wazalishaji chumvi

Lindi. Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (Stamico) imetangaza kuanza ujenzi wa kuchakata chumvi katika Wilaya ya Kilwa ili kupandisha thamani bidhaa hiyo na kuondoa changamoto ya bei ndogo kwa wazalishaji.
Kauli hiyo imetolewa Jumatatu Agosti 21, 2023 na Naibu Waziri wa Madini, Steven Kiruswa katika maonesho ya madini yanajoendelea wilayani Ruangwa mkoani Lindi.
Waziri Kiruswa amesema kumekuwa na malalamiko ya wazalishaji wa chumvi hasa kwa kukosa soko na bei ya kusuasua hali inayosababisha wazalishaji wengi kubaki na chumvi majumbani na kushindwa kujikwamua kiuchumi.
"Tanzania tulikuwa na mnunuzi mmoja wa chumvi, ambae alijinasibu kununua chumvi yote ambayo inazalishwa na wakulima wetu, lakini mwisho wa siku akasema chumvi inayozalishwa na wakulima wetu ni chafu na akaanza kuingiza malighafi ya chumvi kutoka India jambo hili halikubaliki kabisa,"amesema Kiruswa.
Hata hivyo, Kiruswa amesema mpango wa Serikali ni kuwainua wananchi kiuchumi ambapo wizawa hiyo imetoa bei elekezi ya Sh6,000 kwa mfuko mmoja wa kilo 25.
Aidha, Serikali kupitia Stamico imesema itaendelea kuwapa mafunzo wazalishaji ili kuweza kuzalisha chumvi yenye ubora itakayoingia kwenye soko la ushindani la kimataifa.
Kwa upande wake, Meneja Uwekezaji Wachimbaji Wadogo, Tuna Bandoma amesema ili kuzalisha iliyo bora wataendesha mashamba darasa kwa wazalishaji hao.
Katibu wa Uzalishaji Chumvi Tanzania, Julius Mosha amesema bado wanakabiliwa na changamoto ya kukosa masoko na chumvi nyingi inasalia nyumbani kwa wachimbaji.
"Serikali imeamua jambo jema la kujenga kiwanda kwani itatusaidia sisi wazalishaji wadogo kupata soko la uhakika kwani zaidi ya miaka nane chumvi zipo kwenye maghala kwa kukosa soko,"amesema.
Salima Haji, mzalishaji wa chumvi amesema bei ni tatizo linalosababisha chumvi nyingi kusalia ghalani.