Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yaomba Aga Khan kupunguza gharama za afya

Muktasari:

  • Serikali yaiomba jumuiya ya Ismailia nchini kuangalia namna ya kunguza gharama za matibabu zinazotolewa kwenye vituo vya afya na Hospitali za Mtukufu Agha Khan ili kutoa fursa kwa watanzania wote kwenda kupata huduma za afya.

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni ameipongeza Jumuiya ya Ismailia kwa kuendelea kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi, huku akiiomba kuangalia namna ya kupunguza gharama za matibabu zinazotolewa kwenye vituo vya afya na Hospitali za Mtukufu Agha Khan.

Kauli hiyo, ameitoa Dar es Salaam, jana alipokuwa mgeni rasmi kwenye sherehe ya pamoja ya Maulid iliyowajumuisha waumini wa imani mbalimbali, ikiwa ni kuadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Mtukufu Muhammad (SAW).

Msingi wa hoja ya Waziri Masauni, amesema sekta ya afya ni muhimu kwa wote na kuna Watanzania wengi wanatamani kwenda kupata huduma kwenye Hospitali na vituo vya afya vya Mtukufu Agha Khan lakini wanashindwa kwa sababu ya gharama.

"Ni kweli tunatambua kazi kubwa wanayoendelea kuifanya kwa kutoa mchango katika maendeleo ya nchi yetu katika sekta ya afya, elimu, uchumi na sehemu zingine, Watanzania ni mashahidi wazuri wa huduma zinazotolewa na hospitali zao, mfano Agha Khan, moja kati ya Hospitali bora kabisa katika nchi na inatoa mchango mkubwa," amesema Waziri Masauni nakuongeza;

“Nimezungumza namna ya kuangalia kupunguza gharama za matibabu kwa watu ambao hali zao ziko chini, waweze kupata fursa ya huduma nzuri zinazotolewa na hospitali za Mtukufu Agha Khan na baada ya kuongea hivyo nimeona makofi mengi sana inaashiria hata wao wenyewe wanaguswa na umuhimu wa kufanya hivyo," amesema Masauni

Amesema ametoa hoja hiyo na matumaini yake uongozi wa taasisi hiyo utafanyia kazi kwa kuwa imetolewa na aliyeshiriki tukio hilo akimwmwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.

"Nimekuja hapa kwa ridhaa ya kuja kumwakilisha Rais Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa hiyo ni kauli iliyotolewa na mtu aliyemuwakilisha kiongozi mzito wa nchi hii," amesema.

Mwakilishi wa Kidiplomasia wa Agha Khan Development Network Tanzania (AKDA), Balozi Amin Kurji amesema ombi hilo wataangalia lakini afya kwa ujumla nchi zote ukienda lazima uwe na bima ya afya.

"Ukienda bila bima kwenye matibabu inakuwa ghali sana, Na hapa Tanzania kama mliona Bunge limepitisha muswada wa bima ya afya kwa wote, ile itasaidia kwa sababu bila bima itakuwa vigumu kupata matibabu mazuri na ya hali ya juu," amesema Balozi Kurji.

Amesema Tanzania kuna zahanati nyingi tu siyo za Agha Khan pekee lakini ukiona ubora wa huduma lazima kuwepo na gharama fulani ndiyo maana ukienda hospitali za Agha Khan ukilinganisha na zingine lazima utaona utofauti.

"Kwa sababu ya ubora wa huduma na kuna gharama zake lakini hayo yote yanaweza kutatuliwa iwapo wote wana bima ya afya na wanaweza kwenda na bima na wote wakiwa na bima itakuwa jambo nzuri," amesema Balozi Kurji

"Suala la gharama tutaangalia lakini kwa ujumla ukitoa huduma bora lazima gharama ziwe kubwa kidogo na inajulikana," amesema

Amesema Agha Khan wana vituo 32 vya kutoa huduma nchi nzima na kwamba Hospitali ya Aga Khan ni kama hospitali ya rufaa, ambapo mgonjwa hawezi kwenda moja kwa moja bila kupitia kwenye vituo vya afya ambapo ataruhusiwa kwenda katika hospitali hiyo.

"Kama ilivyo Hospitali ya Muhimbili huwezi kwenda moja kwa moja ni mfumo huo huo unatumika Hospitali ya Agha Khan, ukiwa na bima yako ya afya wanalipia gharama zote hamna shida," amesema Balozi Kurji

Akizungumzia sherehe hiyo, Waziri Masauni alianza kwa kuipongeza jumuiya ya Ismailia kwa kuweza kuadhimisha sherehe ya pamoja ya Maulid kwa aina yake kwa  mchanganyiko wa madhehebu mbalimbali ya kiislamu huku akieleza hali hiyo inaashiria kwa vitendo kwa namna gani wanavyodumisha misingi ya amani na upendo kwa watanzania wote.

"Watanzania wenye madhehebu tofauti asili na makabila tofauti, hiyo ni moja ya nguzo ya amani katika nchi yetu, nawapongeza," amesema Masauni.