Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yasitisha mnada wa mitambo Mgodi wa Buzwagi

Dar/Kahama. Serikali imeuagiza Mgodi wa Buzwagi kuahirisha mnada wa mitambo na mashine zake uliokuwa ufanyike leo kutokana na kutokamilika kwa utaratibu wa kuufunga.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila alisema Buzwagi walitoa tangazo la mnada bila kuwasiliana na Serikali, jambo ambalo ni kinyume cha utaratibu.

“Buzwagi walikuja wizarani wakaulizwa maswali kadhaa kuhusu mnada wanaotaka kuufanya, walikosa majibu. Kwa kifupi, hawajafuata utaratibu,” alisema Profesa Msanjila.

Pia, suala la kuahirishwa kwa mnada limezungumzwa na mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Tellack aliyesema: “Ni kweli mnada uliokuwa ufanyike Machi 5 katika Mgodi wa Buzwagi umeahirishwa.”

Tofauti na sekta nyingine, Profesa Msanjila alibainisha utaratibu wa kufunga mgodi wowote nchini kwamba lazima waendeshaji watoe taarifa serikalini kwa kueleza sababu za kufanya hivyo.

Alisema wizara ilipotaka kufahamu ni kwa nini tangazo la mnada limetoka kabla ya mgodi kuwasiliana na Serikali, Buzwagi walikosa majibu hivyo kutakiwa kujibu hoja. “Wamekiri kuwa waliyempa kazi ya kuandaa tangazo alikosea kulitoa mapema, tumewaambia wakalete tangazo lililo sahihi. Huwezi kufunga mgodi kama duka,” alisema katibu mkuu huyo.

Mgodi wa Buzwagi uliopo wilayani Kahama mkoani Shinyanga, unamilikiwa na kampuni ya Acacia ambayo inaendelea na mazungumzo na Serikali kuhusu madai ya ukwepaji kodi tangu ianze shughuli zake nchini takriban miongo miwili iliyopita.

Acacia inadaiwa kukwepa kodi ambayo ikichanganywa na riba na faini inafika dola 190 bilioni za Marekani (zaidi ya Sh425 trilioni).

Katika mazungumzo ya awali yaliyofanyika kati ya Serikali na Barrick Gold Mine, kampuni mama ya Acacia, ilielezwa kampuni hiyo kutoka Canada ilikubali kulipa Sh700 bilioni.

Habari kutoka ndani ya mgodi huo zinasema mnada umezuiwa kutokana na madeni inayodaiwa kampuni hiyo na baadhi ya halmashauri.

Mkurugenzi mtendaji wa Mji wa Kahama, Anderson Msumba alisema halmashauri inaudai Mgodi wa Buzwagi Sh9 bilioni za mapunjo ya ushuru wa huduma yaliyofanywa miaka ya nyuma kwa kuwa tangu uanze uzalishaji ulikuwa ukilipa Sh200 milioni kwa mwaka kabla ya kuanza kulipa asilimia 0.3 ya mapato yake.

Kwa mujibu wa matangazo yaliyotolewa, Buzwagi ilikuwa ipige mnada mitambo, magari na vifaa vingine vya migodini ikiwa ni maandalizi ya kuufunga ifikapo mwaka 2020 kwa madai ya kujiendesha kwa hasara.

Ofisa habari wa Mgodi wa Buzwagi, Blandina Munghezi alisema jana kwamba amesikia taarifa za kuahirishwa kwa mnada, lakini hawezi kusema chochote.

“Nimesikia taarifa hizo lakini nipo likizo. Siwezi kusema chochote.”

Msimamizi wa mnada huo kutoka kampuni ya Harvest Tanzania, Joseph Mambia alikiri umeahirishwa akibainisha kuwa kinachofanyika ni kuwafahamisha wananchi waliotaka kushiriki.

Tayari taarifa za kuahirishwa kwa mnada, Harvest inayoshirikiana na kampuni ya Slattery Auctions ya Australia imeweka tangazo kwenye tovuti yake. Alisema watu kutoka Dubai, Oman, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kwingineko wamejitokeza kushiriki lakini baada ya zuio wanaruhusiwa kukagua mitambo iliyopo na kuondoka.

“Kuanzia Ijumaa mpaka leo (jana) watu wanaendelea kukagua mali zilizopo. Utaratibu utakapokamilika tutatangaza tarehe nyingine ya mnada na watakachotakiwa kufanya ni kuomba kupitia mtandaoni,” alisema Mambia.

Kutokana na mabadiliko yaliyotokea dakika za mwisho kabla ya mnada kufanyika, Mambia alisema baadhi ya washiriki wametishia kuwashtaki kutokana na gharama walizowasababishia.