Serikali yatoa Sh582 milioni ujenzi wa shule mpya ya Sayansi Holili
Mbunge wa Rombo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akizungumza na wananchi wa Kata ya Holili baada ya kufika eneo ambako kutajengwa shule mpya ya masomo ya Sayansi. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Serikali imetoa zaidi ya Sh582 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari itakayofundisha masomo ya Sayansi katika Kata ya Holili, Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro ikiwa ni kuhamasisha na kuongeza idadi ya udahili wa wanafunzi wa kidato cha tano na vyuo vikuu.
Rombo. Serikali imetoa zaidi ya Sh582 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya Sekondari itakayofundisha masomo ya Sayansi katika Kata ya Holili, Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro ikiwa ni kuhamasisha na kuongeza idadi ya udahili wa wanafunzi wa kidato cha tano na vyuo vikuu.
Kujengwa kwa shule hiyo ni moja ya utekelezaji wa mpango wa Serikali katika kuhakikisha kila mkoa unakuwa na shule maalumu za masomo ya sayansi hapa nchini.
Akizungumza na wananchi katika eneo ambalo litajengwa shule hiyo mpya, Kata ya Holili, Mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda amewashukuru wananachi wa Kata ya Holili kwa kutoa eneo kubwa lenye ekari 8 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo, ambapo amesema kukamilika kwa ujenzi huo ambao utaanza hivi karibuni itakuwa ni mkombozi kwa wanafunzi wanaopenda masomo ya sayansi.
Profesa Mkenda ambaye pia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha nyingi katika Wizara hiyo kuhakikisha kila Mtanzania anapata elimu bora na nzuri.
"Namshukuru Rais wetu, Samia Suluhu Hassan, kwa kutenga fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa shule maalum za Sayansi hapa nchini ambapo haya ni maelekezo yake kwamba nchi nzima zijengwe shule hizi na ni dhahiri kuwa fedha zimetolewa na shule zinaendelea kujengwa," amesema.
Diwani wa kata hiyo, Kelvin Kahangala amesema wananchi kwa kuona umuhimu wa ujenzi wa shule hiyo katika maeneo yao waliamua kutoa eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 8 ili shule hiyo iweze kuwanufaisha wananchi wa kata hiyo pamoja na maeneo jirani.
"Tumeweza kupata eneo hili hapa kwa ajili ya ujenzi wa shule yetu mpya ya Sekondari na tumeshawekewa kiasi cha Sh582 milioni kwa ajili ya ujenzi wa shule hii mpya, tunamshukuru mbunge wetu kwa kutupambania na kupata fedha hizi kwa ajili ya ujenzi wa shule hii," amesema.
Nao baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo wamemshukuru Profesa Mkenda kwa namna ambavyo amekuwa akipigania maendeleo ya wilaya hiyo ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya shule katika wilaya hiyo.
Venosa James, ambaye ni mkazi wa Holili, amemshukuru Profesa Mkenda kwa namna anavyopambana kuleta maendeleo katika wilaya hiyo hasa katika sekta ya elimu ambayo imetengewa fedha nyingi za maendeleo.
"Tunaishukuru serikali kupitia mbunge wetu kwa kutujengea shule mpya ya sekondari ya sayansi, hii itaenda kuleta ufanisi mkubwa kwa watoto wetu ambao wanapenda masomo ya sayansi," amesema Venosa.