Sh13 trilioni kutimika kwa maendeleo bajeti 2021/22

Thursday June 10 2021
By Sharon Sauwa

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania  imesema kwa mwaka 2021/22 kiasi cha Sh13.3 trilioni kitatumika  kugharamia miradi ya maendeleo ambayo ni asilimia 37 ya bajeti yote ya Serikali.

Kati ya kiasi hicho Sh6.1 trilioni ni matarajio ya mapato ya ndani na Sh4.1 trilioni ni mikopo ya ndani na nje yenye masharti ya kibiashara na Sh2.9 trilioni ni misaada na mikopo nafuu kutoka nje.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi Juni 10, 2021 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk  Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha bungeni hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2020 na mpango wa maendeleo ya Taifa kwa mwaka wa fedha 2021/22.

Amesema sehemu kubwa ya bajeti ya maendeleo itatumika kugharamia utekelezaji wa miradi ya kielelezo  na miradi mingine ya maendeleo itaendelea kugharamiwa kupitia utaratibu wa ubia kati ya sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) pamoja na utaratibu wa kampuni maalum.

 “Serikali itaendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi kwa kuboresha mazingira ya kufanya

biashara na uwekezaji ili kukuza biashara ndogo na za kati kwa ukuaji endelevu wa uchumi utakaowezesha kupanuka kwa wigo wa kodi pamoja na kuimarisha mazingira ya

Advertisement

ulipaji kodi kwa hiari ikiwemo kuboresha na kuhimiza matumizi sahihi ya mifumo ya Tehama na kutoa elimu kwa umma,” amesema.


Amebainisha kuwa Serikali itaendelea kutekeleza mfumo wa Dirisha Moja la Kielektroniki (TeSWS) ili kurahisisha upitishaji wa mizigo katika vituo vya mipakani pamoja na kupunguza gharama za kufanya biashara nchini, kuendelea kusimamia Mfumo wa Serikali wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato (GePG) pamoja na  kusimamia malipo ya tozo na ada mbalimbali.


Vilevile, amesema serikali itaimarisha usimamizi

wa fedha kutoka kwa washirika wa maendeleo zinazopelekwa moja kwa moja kwenye miradi ya maendeleo kupitia mfumo wa uratibu wa fedha zinazopelekwa moja kwa moja kwa watekelezaji wa miradi ya maendeleo

pamoja na kuimarisha maandalizi ya miradi ya maendeleo.

Advertisement