Shahidi awatambua Sabaya na wenzake ndio waliwavamia dukani

Arusha. Shahidi wa pili katika kesi ya unyang'anyi wa kutumia silaha inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya, Numan Jasin (17) amewatambua kwa kuwashika  mabegani Sabaya na wenzake.


Shahidi huyo ametoa ushahidi huo leo Alhamisi Julai 22, 2021 Mbele ya Hakimu Mkazi, Odira Amworo amesema Sabaya ndiye alikuwa anatoa amri zote, huku mshitakiwa wa pili alimpa simu kutaka apige nyumbani kufungua milango na wa tatu walikaa naye kwenye gari.


Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka shahidi huyo amesema awali wakiwa dukani hakuweza kuwatambua kwani kulikuwa na vurugu dukani.


Shahidi huyo amesema watuhumiwa hao waliwaweka chini ya ulinzi kwa takriban saa tatu kuanzia saa 11 jioni, walipigwa, kusachiwa na kuhojiwa na watuhumiwa hao.


Amesema katika duka hilo walikuwa chini ya ulinzi watu nane, ambao ni yeye, mjomba wake Hajirin Saad, Ally ,Mzee Salimu, Annas, Abuu Mansoor, Bakari Msangi na msichana mmoja.


Jasin amesema baada ya kuwa chini na ulinzi baadaye, waliachiwa wenzao na alibaki yeye na mjomba wake ambao walitakiwa kupanda katika gari lililokuwa nje ya duka.


Hata hivyo amesema mjomba wake ambaye alikuwa amefunga aliomba kununuliwa ndizi ili afungue ndipo Sabaya aliwanunulia ndizi moja moja.


Amesema baada ya kuondoka dukani magari yaliwapeleka nyumbani ambapo wakakuta milango imefungwa ndipo alipewa simu kumpigia mama yake na aliongea na kiarabu kumtaka asifungue.


Amesema baadaye walipelekwa kituo cha polisi Arusha na waliandika maelekezo na kupewa dhamana hadi Februari 10 saa 10 jioni.


Amesema kwa kuwa walimaliza mahojiano usiku polisi aliyekuwa anawahoji aliwapa msaada wa gari lake kuwarudisha nyumbani.
Shahidi huyo wa pili anaendelea kutoa ushahidi wake.

Endelea kufuatilia Mwananchi