SHERIA MSUMENO: Hatima ya Chadema kuamuliwa kesho

Dar es Salaam. Baada ya kusikilizwa kwa zaidi ya miaka miwili sasa, viongozi saba wa Chadema akiwamo mwenyekiti wake Taifa, Freeman Mbowe wanatarajiwa kusomewa hukumu ya kesi ya jinai inayowakabili.

Hukumu hiyo huenda ikabadili maisha yao pamoja na mustakabali wa siasa nchini kwani endapo watakutwa na hatia kwa makosa ya uchochezi yanayowakabili na baadhi yao wakahukumiwa kifungo, basi safu ya uongozi wa chama hicho ngazi ya Taifa ihuenda ikapoteza uthabiti wake.

Wasiwasi huo unaongezeka kwa kuwa mwaka huu ni wa uchaguzi mkuu hivyo iwapo chama hicho kitawakosa viongozi hao kinaweza kutikisika.

Kesi hiyo inawahusu mwenyekiti wa chama, katibu mkuu, viongozi wa kanda, kiongozi wa baraza la wanawake pamoja na wabunge. Kutokana na hali hiyo, wanachama na mashabiki wa Chadema watalazimika kufuatilia kujua kitakachojiri.

Hata hivyo, Mbowe amewataka wanachama wa chama hicho kuwa watulivu akisema wapo tayari kwa hukumu.

“Nataka niwatayarishe wana Chadema, tupo tayari kwa lolote na kama baadhi yetu tutakwenda jela, mliobakia endeleeni kusonga mbele bila woga wala ajizi,” alisema Mbowe jana kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.

Kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni za Adhabu, wanaopatikana na hatia ya uchochezi adhabu yao ni kulipa faini isiyozidi Sh1,000 au kifungo kisichozidi miezi 12 jela au vyote viwili kwa pamoja.

Katika kesi hiyo inayosikilizwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dar es Salaam, Mbowe na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 13 ikiwamo kula njama, mikusanyiko na maandamano yasiyo halali na uchochezi wa uasi.

Mbali na Mbowe ambaye ni mbunge wa Hai, wengine ni katibu mkuu wa Chadema na mbunge wa Kibamba, John Mnyika, naibu katibu mkuu – Zanzibar, Salum Mwalimu na Peter Msigwa, mbunge wa Iringa Mjini na mwenyekiti kanda ya Nyasa Chadema.

Kwenye orodha hiyo, yupo pia mbunge wa Tarime Mjini na mwenyekiti kanda ya Serengeti, Esther Matiko na mbunge wa Kawe na mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (Bawacha), Halima Mdee.

Wengine ni mbunge wa Bunda na mnadhimu mkuu wa upinzani bungeni, Esther Bulaya, mbunge wa Tarime Vijijini na mjumbe wa sekretarieti ya Kamati Kuu, John Heche pamoja na aliyekuwa katibu mkuu kabla hajahamia CCM, Dk Vincent Mashinji.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo Februari 16, 2018 kwenye Viwanja vya Buibui wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kinondoni.

Hukumu ya viongozi hao inatayorajiwa kutolewa kesho inaweza kubadili historia yao endapo ushahidi wa upande wa mashtaka utaishawishi mahakama hiyo na kuwatia hatiani.

 

 SOMA ZAIDI: