Shirika la Maendeleo la Ufaransa: Miaka 25 ya uhusiano wake na Tanzania

Shirika la Maendeleo la Ufaransa: Miaka 25 ya uhusiano wake na Tanzania

Muktasari:

  • Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Stéphanie Mouen yupo nchini tangu mwaka 2018 na hivi karibuni alifanya mahojiano maalum na gazeti hili na kuelezea historia ya shirika hilo tangu mwaka 2008 na na shughuli zake za kimaendeleo kiujumla.

Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Stéphanie Mouen yupo nchini tangu mwaka 2018 na hivi karibuni alifanya mahojiano maalum na gazeti hili na kuelezea historia ya shirika hilo tangu mwaka 2008 na na shughuli zake za kimaendeleo kiujumla.

Unaweza kuwaeleza Watanzania AFD inamaanisha nini?

S.M: “Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) ni taasisi ya pande mbili ya kifedha ya Ufaransa au benki ya umma inayohusika katika utekelezaji wa sera rasmi ya misaada ya maendeleo ya Serikali ya Ufaransa, katika nchi zinazoendelea na zinazokua kwa kasi zaidi.

Kwa kusudi hili, AFD Group imekuwa ikifadhili, kusaidia na kuharakisha mabadiliko kuelekea katika dunia stahamilivu na endelevu, pamoja na washirika wake kutoka nchi 115, kwa lengo la kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s).

Malengo yetu ni; kuboresha upatikanaji wa miundombinu ya msingi na kusaidia maendeleo ya binadamu; kulinda maliasili, bayoanuwai na hali ya hewa thabiti; na kupambania usawa wa kijinsia na afya. Ili kufikia malengo haya, AFD inatoa mikopo ya masharti nafuu kwa Serikali, taasisi za umma na misaada kwa ajili ya shughuli za kiufundi au upembuzi yakinifu.

AFD pia inatoa misaada kwa sekta binafsi kupitia kampuni yake tanzu ya Proparco na kutoa msaada wa kiufundi kupitia wataalamu kutoka Ufaransa.”

Nini ambacho AFD inakifanya nchini Tanzania?

S.M: “Tumekuwa tukifanya kazi na Tanzania kwa miaka 25, awali kwa kutumia ofisi yetu ya Nairobi nchini Kenya, na baadae moja kwa moja kutoka katika ofisi yetu ya Dar es Salaam ambayo ilifuguliwa rasmi mwaka 2008.

Kihistoria, AFD hapa Tanzania imejikita katika kufadhili miundombinu. Tangu 2009, tumejikita kushughulikia maeneo ya kipaumbele yaliyotambuliwa na Serikali, kwa hivyo tumefanya kazi zaidi katika sekta ya nishati (sekta hii inachangia asilimia 47 ya shughuli zetu), maji (asilimia 28) na sekta za uchukuzi (asilimia 19).

Mifano ya matokeo halisi ya shughuli zetu ni kama ifuatavyo:- » Kuboreshwa kwa upatikanaji wa umeme huku watumiaji wa nishati hiyo zaidi ya watu 150,000 kutoka maeneo ya vijijini wakifaidika na uboreshaji mkubwa wa huduma ya umeme, kilomita 750 za njia mpya za usambazaji umeme zikifikiwa nchi nzima; Katika eneo la Ziwa Victoria, watu milioni 4 sasa wananufaika na upatikanaji bora wa maji safi kwa matumizi ya binan-damu na takribani watu milioni 1 wanapata hudu-ma endelevu ya usafi wa mazingira katika mikoa ya Bukoba, Musoma na Mwanza; Upanuzi wa Hospitali ya Aga Khan (Huduma za Hospitali ya Aga Khan) jijini Dar es Salaam na kuanzishwa kwa vituo vipya 30 vya afya kote nchini.

Na orodha hii haiishii hapo!

Shughuli za AFD nchini pia zimejikita katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi: zaidi ya nusu ya miradi ambayo tumeifadhili tangu 2008, ilikuwa na matokeo chanya dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Programu hizi pia zinajenga uwezo kwa mashirika yanayotekeleza miradi hiyo ili kuhakikisha uendelevu wa miradi.”

Vipaumbele vya AFD vijavyo ni vipi?

S.M: “Tumeongeza kiasi cha msaada wetu kwa Tanzania mara dufu zaidi kati ya mwaka 2017 na 2021 hadi kufikia wastani wa Sh420 bilioni (sawa na Euro 150 milioni) kila mwaka, kwa miaka 3 iliyopita. Na tunakusudia kuendelea na mfumo huu kwa vile Tanzania ni nchi yenye tija kubwa na ni mshirika wa Ufaransa / AFD.

Kwa miaka ijayo, mkakati wetu ni kuendeleza uboreshaji wa huduma za maji na usafi wa mazingira, nishati na uchukuzi, sambamba na vipaumbele vya Tanzania. Pamoja na hayo, tunakusudia pia kuelekeza fedha zetu katika sekta zingine kama vile; kilimo endelevu kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi, uhifadhi wa mazingira, uhifadhi na mbuga za kitaifa, Uchumi wa Bluu na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).