Shirika lakabidhi darasa, maabara chuo cha afya Mpanda

Wanachuo wa chuo cha afya na sayansi shirikishi Mpanda wakiwa ndani ya darasa lililojengwa na shirika la Christian Social Service Commission (CSSC). Picha na Mary Clemence

Muktasari:

  • Shirika la Christian Social Services Commission (CSSC) wakabidhi darasa na maabara katika chuo cha afya Mpanda ili kupunguza changamoto ya upungufu wa madarasa.

Katavi. Chuo cha afya na sayansi shirikishi Mpanda kimekabidhiwa darasa na maabara na Shirika la Christian Social Services Commission (CSSC), ikiwa ni juhudi za kupunguza changamoto za upungufu wa miundombinu na vifaa katika chuo hicho.

Akisoma risala kwenye hafla ya makabidhiano ya majengo hayo leo January 14, Mkuu wa chuo hicho Lightness Maico amesema chuo hicho pia kinakabiliwa na tatizo la upungufu wa vitabu vya kufundishia, ofisi za walimu jambo alilosema linawaathiri kiutendaji.


"Tunao wanachuo 119 na walimu waliopo ni 10, kati yao saba ni wa kudumu na watatu ni wa muda, hivyo hawatoshi,” amesema Lightness.

Amsema chuo hicho kilianzishwa mwaka 1974, lakini mwaka 1996 kilisitisha huduma hadi Wizara ya Afya ilipofanya jitihada kikafunguliwa 2020 kikianza na wanachuo 50 na sasa wameongezeka.

Akizungumzia msaada huo, mwakilishi wa maaskofu kutoka shirika la CSSC, Askofu Eusebius Nzigirwa amesema ni moja ya huduma wanazotoa katika jamii.

"Tumejenga darasa jipya linachukua wanachuo 102 na maabara tumeikarabati imekuwa ya kisasa vyote vinagharimu Sh236 milioni

"Shughuli hii tuliyofanya ni wito uliotoka kwa Mwenyezi Mungu kumhudumia mwanadamu kiroho na kimwili," amesema Askofu Nzigirwa.

Naye Meneja wa benki ya NMB kanda ya Magharibi, Sospeter Magese amesema wao wamekabidhi meza 100 na viti 100 vyenye thamani ya Sh10 milioni.


"Vitatumiwa na wanachuo kwenye darasa lililojengwa na wenzetu CSSC. Hii ni kutokana na asilimia moja tunayotenga kila mwaka na kuielekeza kwenye huduma za jamii hususani afya na elimu," amesema Magese.

Katika hotuba yake Mkuu wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko baada ya makabidhiano hayo amewashukru wadau kuendelea kuchangia shughuli za maendeleo.

"Niipongeze Wizara ya Afya kuwezesha chuo hiki kuanza kufanya kazi. Sisi kama mkoa tutashirikisha mamlaka husika walimu wapatikane," amesema Mrindoko.

Akizungumza kwa niaba ya wanachuo, Ester John amesema wanaishukru serikali na wadau kwa hatua hiyo ya kurejesha huduma za masomo chuoni hapo.