Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simanzi yatanda, miili 11 ya waliofariki kwa ajali Arusha ikiagwa

Muktasari:

  • Ajali hiyo ya barabarani ilihusisha magari manne likiwamo lori lililopata hitilafu kwenye mfumo wa breki, Februari 24, 2024 eneo la Kibaoni (Ngaramtoni), Arusha.

Arusha. Simanzi imetawala katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid, baada ya kuwasili miili ya watu 11 kati ya 25 waliofariki dunia katika ajali ya barabarani ikiwamo ya watoto wadogo watatu.

Leo Jumanne Februari 27, 2024 Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Pindi Chana ameongoza waombolezaji kuaga miili hiyo.

Watu hao walifariki dunia katika ajali ya barabarani iliyohusisha magari manne likiwamo lori lililopata hitilafu kwenye mfumo wa breki, Februari 24, 2024 eneo la Kibaoni (Ngaramtoni), Arusha.

Miongoni mwa wanaoagwa leo ni watoto watatu, wawili kati yao wakiwa ndugu. Pia yupo mama na mtoto wake.

Watoto ambao ni ndugu ni Cathbeth Johnson mwenye miaka saba na Garson Johnson (18).

Pia wamo Neema Loserian (44) na mwanaye Dorcas Loserian mwenye miaka miwili.

Wengine ni Joseph Muna (33), Elias Lukumay (27), Queen Lomayan (28), Judith Daud (34), John Mukolwe na Elias Saning'o.

Mwili mwingine ni wa Obeid Zakayo (40) ambaye alikuwa dereva wa basi la Shule ya Mchepuo wa Kiingereza ya New Vision.

Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Missaile  Musa, amesema katika tukio hilo wamefariki watu 25 wakiwemo raia 10 wa kigeni.

Amesema baada ya ajali, majeruhi 21 walilazwa hospitalini, kati yao wanaume walikuwa 14 na wanawake saba.

Musa amesema majeruhi hao 11 walilazwa Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, St Joseph (3), Selian Ngaramtoni (4), Selian mjini (2) na Olturmet mmoja. Kati ya hao amesema tisa ni raia wa kigeni.

Amesema majeruhi watano kati yao wanne raia wa kigeni na mmoja Mtanzania wanaendelea kupatiwa matibabu.

Musa amesema mmoja amepewa rufaa katika Hospitali ya KCMC na mwingine raia wa Kenya ameenda kutibiwa nchini humo baada ya Taifa hilo kuomba akatibiwe huko.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Maridhiano Tanzania, Askofu Israel Maasa amesema: “Mambo haya (ajali) yanapotokea hatuwezi kuhesabu ni laana na kuwa moja ya mambo ambayo Mungu amefanya usiri ni pamoja na kifo.”

"Mungu ni Mungu wa siri na ana mambo ambayo ni wazi kwake ila kwa dunia ni siri kubwa, moja ya usiri wa Mungu ni lini na jinsi gani tutakufa," amesema Dk Maasa.

Amesema, "Hata yanapotokea mambo kama haya hatuwezi kuhesabu ni laana ya Mungu, tuhesabu ni usiri wa Mungu. Mlioguswa sisi kama viongozi wa dini kuna usiri wa Mungu katika kifo, tupokee hili kama usiri wa Mungu katika upendo wake."

Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Mount Kilimanjaro, Dk Stanley Hotay, amesema ajali hiyo ni janga, familia zinalia.

"Hili ni janga halikutarajiwa bali limetukuta wana-Arusha, tumepigika mauti ya halaiki ni magumu sana, aondokapo mtu duniani damu yake inalia hainyamazi tunasikitika kwa yaliyotokea," alisema Askofu Hotay.

"Tunaweza kulaani dereva aliyesababisha ajali, kufeli breki katika gari si kosa la dereva, tunaweza kusema kwa nini hakuangusha kwenye mtaro? Tunasikitishwa na mambo yaliyotupata hatujui kwa nini ila Mungu anajua," amesema.