Simulizi familia ilivyonusurika ajali ya treni

Muktasari:

  • Mkazi wa Kariakoo manispaa ya Tabora, Nashon Mfanye ameeleza namna uamuzi wa kutosafiri pamoja katika treni iliyopata ajali ulivyoinusuru familia yake.

Tabora. Mkazi wa Kariakoo manispaa ya Tabora, Nashon Mfanye ameeleza namna uamuzi wa kutosafiri pamoja katika treni iliyopata ajali ulivyoinusuru familia yake.

Akizungumzia leo Ijumaa Juni 24, 2022 kuhusu ajali hiyo iliyosababisha vifo vya watu wanne na kujeruhi 132, Nashon amesema ilikuwa wasafiri kwa treni ya abiria yeye na ndugu zake watatu na watoto watatu.

Amesema kuna mtu aliwashauri kutosafiri wote kwa kutumia usafiri mmoja wa treni na ndipo walipoamua kugawana kwa kutumia usafiri tofauti.

"Mimi na ndugu yangu tuliamua kupanda basi na kuwaacha dada zangu Zekerina na Adelina kupanda treni kwa vile walikuwa na watoto," amesema.

Ameeleza kuwa wakiwa wanaelekea Urambo kutoka Kaliua, wakawasiliana kwa mara ya mwisho kabla ya ajali kutokea.

Amesema Zekerina na Adelina walijeruhiwa katika ajali hiyo iliyowanusuru watoto wao na leo Adelina Mfanye amesafiri na mtoto wake kwenda Dar es Salaam.

Kuhusu Zekerina, amesema aliamua kumtoa hospitali ya Kitete, "niliona awe anaugulia nyumbani kwangu na tumeambiwa turudi baada ya siku saba. Hali yake si nzuri na nilimtoa hospitali kutokana na huduma za pale maana majeruhi ni wengi. Dada yangu aliumia kichwani na kifuani."

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao ameeleza kuwa treni hiyo iliondoka Kigoma ikiwa na abiria 582 na kuongezeka njiani hadi kufikia 900  wakati inapata ajali.

Abiria wengi walisafirishwa kuendelea na safari usiku kwa mabasi na treni ya abiria kutoka Mwanza.

Mkazi wa Kariakoo, Manispaa ya Tabora, Nashon Mfanye

Mkuu wa mkoa wa Tabora, Dk Batilda Burian alieleza kuwa mabasi saba na mabehewa ya treni ya abiria kutoka Mwanza ulitumika kuwasafirisha abiria waliokuwa kwenye treni iliyopita ajali.