Simulizi ya waliorejea shule baada ya kutoka kujifungua

Mary Kinunda
Muktasari:
Pia wapo wavulana waliocha shule kwa vishawishi potofu.
Ruvuma.“Niliumia sana moyoni baada ya kuwaona wenzangu wakivaa sare na kwenda shule kusoma wakati mimi nikirandaranda mtaani.” Hiyo ni kauli ya Mary Kinunda, anayesimulia mkasa na majuto yake baada ya kupata ujauzito mwaka 2021.
Akiwa mmoja kati ya watoto watano wa familia ya Gotamu Kinunda, Mary alipata ujauzito akiwa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya wasichana Mbinga na wakati huo alikuwa hajafikisha umri wa miaka 18.
“Sikuwaza kufanya kitu tofauti, bali nilijutia kosa langu na nilichokuwa nakisubiri ni kujifungua salama, ili nirejee shuleni kuendelea na masomo.
“Namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kuruhusu wanafunzi waliokumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ujauzito kurejea shuleni,” anasema Mary.
Novemba 24 mwaka jana, Serikali ilitangaza kuruhusu wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito kurejea shule katika mfumo rasmi baada ya kujifungua.
Pia, wanafunzi wa shule za msingi wanaoshindwa kufaulu mitihani ya kuhitimu elimu hiyo nao watakuwa na nafasi ya kurudia mitihani kama ilivyo kwa wenzao wa kidato cha nne na tano.
Uamuzi huo wa Serikali ulipokelewa uliungwa mkono na wadau wa elimu na maendeleo ambao kwa muda mrefu walikuwa na shauku wa kuitaka Serikali kulegeza msimamo wake kuhusu wanafunzi wanaopata ujauzito wakitaka waruhusiwe kurudi shule.
Mwananchi ikizungumza na Mary anayeishi kata ya Mkumbi katika halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, anasma baada ya kupata ujauzito na kukiri kosa kwa wazazi wake, walimtaka asikate tamaa, badala yake ajitunze huku akitambua kuwa ipo siku atarejea shuleni. Anasema alipitia wakati mgumu baada ya kupata ujauzito, kwani majirani walimtazama vibaya, huku wakimnyooshea kidole kwa kitendo hicho.
Msichana huyo anasema mwanaume aliyempa mimba alimtelekeza, lakini anamshukuru baba yake, Kinunda kuwa mstari wa mbele katika kumhudumia hadi alipojifungua salama.
“Mzazi mwenzangu nilikutana naye baada ya yeye kutoka mgodini, haikuwa kazi rahisi kukubali kuingia kwenye uhusiano, lakini kila nilipokutana naye aliniambia ananipenda, nilikumkatalia lakini sijui ikawaje hadi matokeo yake kama hivi.
“Katika pitapita zangu siku moja ghafla nikajikuta naingia kwenye anga zake, baada ya kushika ujauzito na kujifungua sikumuona tena hadi leo, kwa sasa mwanangu ana umri wa miezi sita,” anasema Mary.
Mary anasema alipata ujauzito akiwa nyumbani katika mapumziko ya likizo fupi, aliporudi shuleni alibainika kuwa mjamzito, ndipo alipoamuliwa kukatisha masomo yake.
“Sikudhamiria kupata ujauzito ulionisababishia nikae nyumbani mwaka mmoja bila kuendelea na masomo. Najiulaumu hadi leo, nakubali nilifanya makosa makubwa,” anaeleza Mary.
Anaeleza baadhi ya wasichana wanaopata mimba wakiwa shuleni wanafikiria kuitoa, ili kukwepa aibu lakini kwake ilikuwa tofauti, aliamua kuwashirikisha wazazi wake ambao walimshauri azae.
“Sitosahau wakati najifungua Ivan nilipitia maumivu, lakini nashukuru Mungu ilikwenda salama, maana nilikuwa bado sijafikisha umri wa kuzaa. Kwa sasa mwanangu anaendelea vizuri,” anasimulia msichana huyo.
Kuhusu uamuzi wa serikali
“Taarifa ya wanafunzi kuruhusiwa kurejea shuleni nilizipokea kwa furaha wakati huo. Baada ya kusikia nikamuuliza baba kama amesikiliza taarifa ya habari, nikamwambia ikifika saa 2 usiku fungulia runinga uangalie.
“Baba aliangalia taarifa ya habari na na kumshukuru Rais Samia kwa uamuzi huu, akaniambia sasa ni wakati mimi kurejea shuleni, nilitamani shuleni zifunguliwe mapema, ili niripoti,”anasema Mary.
Licha ya kutokuwa na mawasiliano ya karibu na mzazi mwenzake, anasema anaamini Mungu atamsaidia mwanaye alelewe na kukua vizuri.
“Mungu atanisaidia na ndoto zangu zitatimia na Ivan atalelewa na wazazi wangu,”anaeleza Mary kwa sauti ya upole huku akilengwa na machozi.
Anasema anamshukuru baba yake kwa malezi kwa mtoto wake huku akimuahidi kutomuangusha katika masomo yake baada ya kurejea shuleni. “Nitahakikisha ninamaliza masomo yangu ya kidato cha nne kwa ufanisi, hii ni ahadi kwa baba yangu na Serikali iliyoamua kutoa ruhusa kwa wanafunzi waliopata ujauzito kurejea shuleni. Natamani nifike hadi kidato cha sita na hatimaye chuo kikuu,” anasema Mary.
Baba afunguka
Baba mzazi wa msichana huyo, Kinunda anasema alipokea taarifa za mwanaye kuwa mjamzito baada ya kupigiwa simu na mkuu wa shule ya Mbinga.
“Nilipopata taarifa hizonilichanganyikiwa sana…niliambiwa sina ujanja niende shuleni nikamchukue mwanangu., nilisikitika sikuweza kupata majibu kwa muda wa dakika 10. Baada ya kuwapa taarifa ndugu zangu walinishauri na kunituliza.
“Nilikwenda kutoa taarifa kwa mtendaji kata na polisi walioniahidi kumtafuta kijana aliyempa mimba binti yangu. Hata hivyo, baada ya kusikia taarifa hizi alitoweka. Baada ya kumsikiliza kwa makini binti yangu nilimuona ana upeo wa kuendelea na masomo, jambo hili lilinipa ahueni,” anasema Kinunda.
Kinunda anasema wakati akitafakari namna ya kumuendeleza kimasomo binti yake, alisikia tangazo la Serikali kuhusu wanafunzi walioshika ujauzito kurejea shuleni. “Naishukuru Serikali kwa uamuzi huo, wakati wowote Mary ataendelea na masomo yake,” alisema. Ofisa Elimu Sekondari wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Peter Ntalamila anasema wapo tayari kuwapokea wanafunzi waliokumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo ujauzito, akitolea mfano kwa Mary ambaye taratibu zake zipo mbioni kukamilika, ili kuendelea na masomo katika Shule ya Sekondari Mbinga.
“Baada ya kupata agizo na Serikali tumeshaanza mchakato wa kushirikiana na wakuu wa shule pamoja na viongozi wa kata na vijiji. Kupitia wakuu wa shule tunapata majina ya watoto walioacha shule kwa sababu mbalimbali.
“Tuna orodha yote na tunachokifanya tunawasiliana na wazazi, kama ikishindakana tunapitia uongozi wa kijiji, ili mwanafunzi atafutwe kokote alipo. Hadi sasa tumeshapata watoto wanne ambao wazazi wao wameomba waendelee na masomo baada ya tangazo la Rais Samia,” anasema Ntalamila.
Mwingine arudi shule
Mbali na Mary, Mwananchi pia ilizungumza na Abdul Kabwea (13) anayeishi kijiji cha Mandepwende wilayani Natumbo, aliyekatisha masomo baada ya kupata vishawishi kutoka kwa marafiki zake.
Sasa amerejea shuleni kutokana na uamuzi wa Serikali na maboresho mbalimbali ya miundombinu ya madarasa yaliyofanyika.
Kabwea aliyekatisha masomo akiwa darasa la saba katika shule ya Mandepwende, amerejea kuendelea na masomo baada ya Serikali la kuruhusu watoto walioacha shule kutokana na changamoto mbalimbali kurejea shuleni.
“Nilishawishia mtaani na vijana wasiosoma, ilikuwa Julai mwaka jana ambapo waliniambia cheti si cha muhimu na niache shule. Muda ambao sikuwa shuleni nilienda shamba, lakini sasa hivi nimejutia kosa langu nimeamua kurudi shuleni kwa sababu cheti ni muhimu kwa manufaa yangu kwa maisha ya baadaye ,” anasema Kabwea.
Kabwea anasema baada ya kurejea shuleni alipokelewa vizuri na wanafunzi aliowakuta, akisema anapewa ushirikiano wa kutosha katika masomo.
Mohamed Makale ambaye ni babu wa Abdul, anasema mjukuu wake aliacha shule kutokana na utoro na vishawishi kutoka kwa marafiki zake, lakini baada ya wenzake kufanya mtihani wa kumaliza darasa la saba alikaa na kujiuliza kwa nini hakumaliza masomo yake ya elimu ya msingi.
“Baada ya kuacha shule muda mwingi alikuwa akifanya shughuli mbalimbali za mitaani, ikifika mahali alijutia kosa la kuamua kutaka kurudi shule hasa ukizingatia maboresho ya miundombinu ya madarasa.Tamko la Rais Samia kuruhusu watoto kurejea shuleni limetufurahisha wazazi.
“Hata mimi natamani kurejea shuleni kama umri ungekuwa unaruhusu maana madarasa mazuri yana viti na meza za kutosha,” anasema Makale.