Sintofahamu Kanisa Anglikana, Dk Mokiwa adai mafao

Aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa

Muktasari:

  • Aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa amelalamika kunyimwa stahiki zake baada ya kuondolewa kwenye nafasi hiyo.

Dar es Salaam. Aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa amelalamika kunyimwa stahiki zake baada ya kuondolewa kwenye nafasi hiyo.

Dk Mokiwa alivuliwa uaskofu mkuu Januari 7 mwaka 2017 na aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk Jacob Chimeledya kutokana na mashitaka 10 aliyofunguliwa na walei 32 wa kanisa hilo yakiwamo ya ufisadi wa mali.

Hata hivyo, ni miaka sita sasa imepita tangu uamuzi huo ufanywe na nafasi ya Dk Mokiwa kuzibwa na Askofu Jackson Sosteness lakini anadai kuwa hakuna stahiki yoyote aliyopata kama ilivyo utaratibu wa kanisa hilo ambao pia unaotumika kwa maaskofu wengine waliowahi kulitumikia.

Kupitia mitandao ya kijamii tangu juzi jioni, lilisambaa andiko la Dk Mokiwa alilolielekeza kwa Askofu Jackson akilalamikia stahiki anazodai hajazipata tangu kuondolewa kwenye nafasi hiyo.

Akizungumza na Mwanachi jana, Dk Mokiwa alisema amefanya jitihada mbalimbali kuwasiliana na Askofu Jackson kupata stahiki zake lakini, hajafanikiwa licha ya hali yake kwa kiafya kwa sasa kuzidi kuwa mbaya.

Alisema licha ya kufuata utaratibu unaoelekezwa na kanisa kupitia ngazi mbalimbali ikiwamo kumwandikia barua Askofu Jackson na halmashauri ya kudumu ya dayosisi ambayo ndiyo mwajiri, bado anapigwa danadana.

“Sikuishia hapo nililifikisha suala hili kwa Askofu Mkuu wa Anglikan, Maimbo Mndolwa ambaye alimwandikia barua Askofu Jackson anilipe posho zangu na stahiki nyingine tangu Agosti 17 mwaka 2018, lakini hadi leo hakuna nilichopata na afya yangu inazidi kuzorota na inanishangaza haya kufanywa na kiongozi wa dini.

“Naumwa shinikizo la damu, ugonjwa wa moyo na kisukari, natakiwa kuchoma sindano za insulin kila baada ya saa 24 hadi 48, kuna wakati nakosa sindano kwa sababu sina fedha kupata dawa hiyo, naumia napitia haya wakati kuna mtu amekalia stahiki zangu, je hadi nife ndiyo nipate haki zangu?,” alihoji Mokiwa na kuongeza: “Nimeamua kusema wazi maana sioni sababu ya kuendelea kulifanya suala hili siri wakati nazidi kuumia, mimi ni mtu mzima nimejitahidi kulishughulikia ila naona mwenzangu hajali na huenda hana mpango wa kunilipa stahiki zangu, nimeona niseme ili kama nastahili, anilipe.”

Mwananchi inayo nakala ya barua iliyosainiwa na Askofu Mndolwa ikielekeza kulipwa kwa stahiki za Dk Mokiwa.

“Tangu Askofu Mokiwa alipoondoka madarakani hadi sasa hajapata posho zake stahiki kama askofu mstaafu. Kwa kuwa ana familia na ni mgonjwa, tunakuandikia kukukumbusha kuwa ni wajibu wa maaskofu tuliomo kazini kuwaenzi na kuwatunza waliotutangulia. Ni imani yetu atalipwa stahili zake zote ambazo ni usafiri, nusu ya posho aliyokuwa akiipata akiwa madarakani na makazi,” inasomeka sehemu ya barua hiyo.

Akizungumzia madai hayo jana, Askofu Jackson alisema kanisa lina mifumo yake, hivyo Dk Mokiwa anapaswa kuizingatia na kuifuata kama inavyoelekeza.

“Kama kuna jambo anadhani hakutendewa haki, kanisa lina mifumo yake ni imani yangu kanisa haliwezi kumdhulumu, afuate hatua zinazostahili kupata hicho anachokihitaji.

“Anaifahamu mifumo kama mimi ambavyo ninaifahamu ndiyo maana sitaki kutumia njia aliyoitumia yeye licha ya kuwa nimeyaona malalamiko yake kwenye mitandao ya kijamii.

“Mimi siwezi kuwa mkubwa zaidi ya kanisa au mifumo ya kanisa, nisingependa kulizungumzia zaidi suala hili, itoshe kusema kanisa lina mifumo yake, aifuate,” alisema Askofu Jackson.