Siri wizi wa transfoma za Tanesco

Transfoma za Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), zilizokamatwa maeneo ya Pugu jijini Dar es Salaam zikiwa ndani ya fuso lililoegeshwa katika kituo cha polisi Chanika.

Muktasari:

  • Kuiba transfoma za umeme ni kosa la jinai na linaweza kuwa na madhara makubwa, si tu kwa mtu binafsi anayefanya wizi huo, bali pia kwa jamii nzima ikiwamo kukosekana kwa  huduma za umeme.

Dar/Moshi. Kutokana na wizi wa transfoma 85 unaotajwa kuchangia kukosekana kwa umeme katika baadhi ya maeneo nchini, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limesema thamani ya hasara iliyopatikana kutokana na wizi huo ni takribani Sh500 milioni.

Taarifa kuhusu wizi wa transfoma hizo, iliwekwa wazi bungeni jijini Dodoma juzi na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, alipokuwa akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali kuhusu umeme, akisema idadi aliyoitaja ni wizi uliofanyika Januari pekee.

Dk Biteko, ambaye alikuwa akichangia taarifa ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini alisema jitihada zinafanyika kuhakikisha wizi huo unakomeshwa, na wanaobainika hatua kali zinachukuliwa.

Kwa mujibu wataalamu wa umeme, nchini tunatumia transfoma za kilovoti (KVa) 25, 50, 100, 200, 300, 500 ambazo uzito wake ni kati ya kilo 340 hadi tani 1.8.

Mfano transfoma ya KVa 25 uzito wake ni kilo 340, kimo chake ni mita 0.65, urefu wake ni mita 0.9 na upana mita .9 huku transfoma ya KVa 500 uzito wake ni tani 1.8, kimo chake ni mita 1.7, urefu wake ni mita 1.7 na upana wake ni mita 0.95.

Ili kuibeba transfoma ndogo kabisa ni lazima uwe na gari lenye winchi ambapo itafungwa kamba ili kuishusha au kama ni watu kuibeba, lazima wawe wanne au watano.

Kutokana na ugumu uliopo wa kuiba transifoma ambayo muda mwingi inakuwa na umeme ambao ni hatari, wapo wanaohusisha wizi wa vifaa hivyo na watumishi wa shirika hilo, wakihoji inawezekanaje mtu asiyefahamu masuala ya umeme aiibe?

“Wanaozifungua transfoma ni wenye kampuni zinazojihusisha na ujenzi wa laini za umeme au watu binafsi wanaojihusisha na vitu vya umeme, ambao wakishazichukua wanakwenda kuziuza kwa hao wasambazaji.”

“Na ili uifungue, kwanza huwezi kuwa mtu mmoja na lazima wawasiliane na watu waliozijenga, kama ni Kibaha wanatafuta mwenyeji anayehusika na eneo hilo ambao ni Tanesco au Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), ndiye  anawaelekeza nendeni kafungueni  eneo fulani,” amesema mmoja wa wafanyakazi katika kampuni ya usambazaji umeme vijijini aliyeomba hifadhi ya jina lake.

Mfanyakazi huyo wa kampuni ya usambazaji wa umeme, amesema, “wakishafungua (hao wanaoiba) wanakwenda kuwauzia kampuni zinazojenga sehemu nyingine, wanachokwepa ni kununua transfoma mpya.

Amesema kiwandani transfoma zinaanzia Sh15 milioni hadi Sh30 milioni, “sasa anaona kwa nini atoe Sh20 milioni au Sh30 milioni wakati anaweza kupata kwa Sh5 milioni au Sh10 milioni.”

“Kwa hiyo katika hili la wizi wahusika ni wenyeji kwa sababu wanakwenda kama kuzifanyia matengenezo, wanaifungua na kuondoka nayo na hata wananchi wakiona wanadhani wanatengeneza, kumbe ndio wanaziiba,” amesema.

Naye mmoja wa wataalamu wa umeme aliyewahi kufanya kazi Tanesco aliyeomba hifadhi ya jina lake amesema, kuna transifoma za Kv50, Kv100, Kv200, Kv300, Kv500, Kv25, Kv1000, “inategemea inalisha watu wangapi, inawekwa kutokana na mahitaji.”

Alipoulizwa transfoma ikiibwa Dar es Salaam haiwezi kutambulika hata ikipelekwa maeneo mengine kufungwa, amesema,“haiwezi kujulikani, kwa kuwa namba za utambulisho wakishaiiba wanazibadilisha na kwa kuwa kiumbo na mwonekano zinafanana inakuwa ngumu sana kuitambua.”

Dar, Pwani vinara wizi wa transfoma

Chanzo hicho kimeeleza kwamba Tanesco inapoagiza transfoma zake, huwekwa kibati cha  kuonyesha kuwa ni mali yao, “kibati hicho, hubadilishwa na kuwekwa cha kampuni nyingine, kwa hiyo namba ya utambuzi na kibati vikibadilishwa huwezi kujua.”


Walichokisema Tanesco

Akizungumzia wizi huo jana, Msemaji wa Tanesco, Kenneth Boymanda amesema kinachoibwa si transfoma yote kama wengi wanavyodhani, bali ni vifaa ndani ya mtambo huo.

“Wezi hawaibi transfoma yote, hapana. Ndani ya transfoma kuna kopa, hiyo ndiyo inayoibwa, au mafuta lakini wezi wa mafuta wamepungua kwa sasa ni kopa,” amesema.

Ameeleza kopa hiyo inakwenda huuzwa na hata hivyo haina gharama kubwa kama inavyodhaniwa, ni kiasi kidogo cha fedha kati ya Sh15,000 hadi Sh20,000.

Hata hivyo, amesema tayari timu ya usalama wa miundombinu ya shirika hilo kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama inaendelea na upelelezi kubaini waliohusika.

Amesema uchunguzi unaendelea kufanyika kubaini wezi ni kina nani na wanauzia wapi hicho wanachokiiba, ili mtandao wote udhibitiwe.

Alipoulizwa kuhusu hasara, amesema inawakumba wananchi na Tanesco kwa ujumla.

Kwa upande wa wananchi, amesema transfoma moja inahudumia kati ya wananchi 50 hadi 200, hivyo ikiharibiwa wote hao watakosa huduma.

Kwa upande wa Tanesco, ameeleza hasara inakuja pale zinapohitajika fedha kwa ajili ya ununuzi wa transfoma nyingine ili kuendelea kutoa huduma kwa wananchi.

Kwa transfoma hizo zilizoibiwa, hasara yake ni takribani Sh500 milioni.

Hata hivyo, amesema wizi wa vifaa hivyo hutekelezwa na watu wenye ujuzi kiasi wa umeme, kwa kuwa ili uibe kifaa hicho inabidi ukitoe kwenye nishati hiyo.

“Kuwa na ujuzi wa umeme haimaanishi eti uwe mtumishi wa Tanesco. Siku hizi kuna vyuo vingi vya umeme, lakini kuna wale vibarua leo anachimba shimo, kesho akipata ujuzi kama si mwaminifu anaweza kuja kuiba,” amesema.


Kilimanjaro.

Katika hatua nyingine, mkoani Kilimanjaro wafanyakazi  17 wa Tanesco wanashikiliwa na Jeshi la Polisi wakituhumiwa kujipatia zaidi ya Sh8 milioni kwa kuwaunganishia watu 21 umeme kinyemela.

Kulingana na Kamanda wa Polisi Kilimanjaro, Simon Maigwa wananchi hao wanaoishi Kibosho wilayani Moshi, inadaiwa kila mmoja alitozwa Sh400,000 kuunganishiwa huduma hiyo.

Hata hivyo, amesema tayari watu hao wamekamatwa na miongoni mwao, yupo kinara anayedaiwa kuwa kiongozi wa vishoka mkoani humo.

"Tumeshamkamata kiongozi wao mkubwa wa hicho kikosi, amekuwa akishirikiana na mtandao mkubwa uliopo ndani ya watumishi wa Tanesco, wote hawa tumewakamata na tuko kwenye hatua nzuri," amesema Maigwa.

Akizungumzia hilo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kisare Makori amesema watu hao wamekuwa wakiihujumu Serikali kwa manufaa yao binafsi na kuikosesha mapato.

Amesema hadi sasa watu 21 maeneo ya Kibosho, wilayani humo wamefungiwa umeme kinyume na taratibu na kila mwananchi alilipishwa Sh400,000 na fedha hizo haziingi serikalini.

Alipotafutwa Meneja wa Tanesco mkoani hapa, Grace Ntungi kuhusiana na kukamatwa kwa wafanyakazi wa shirika hilo, amesema hawezi kuzungumia suala ambalo lipo kwenye upelelezi na kwamba viachiwe vyombo vya dola   viendelee na kazi yake.

"Hizi taarifa zipo chini ya uchunguzi wa Jeshi la Polisi, taratibu za uchunguzi zitakapokamilika tutatoa pia taarifa, ili tusije vuruga taratibu za Jeshi letu la Polisi," amesema meneja huyo.