Stendi ya Nyegezi yakamilika, yaanza kutumika kwa muda

Muonekano wa stendi kuu mpya ya Nyegezi jijini Mwanza. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

Pamoja na mradi wa ujenzi wa stendi mpya ya kisasa eneo la Nyegezi kwa gharama ya zaidi ya Sh15.8 bilioni, Halmashauri ya Jiji la Mwanza pia inatekeleza mradi wa ujenzi wa Soko Kuu kwa gharama ya zaidi ya Sh20.7 bilioni

Mwanza. Stendi Kuu mpya ya Nyegezi jijini Mwanza imeanza kutumika kwa majaribio kuanzia Jumatatu Juni 5, 2023 kabla ya hafla ya uzinduzi rasmi utakaofanyika Juni 9, 2023.

Utekelezaji wa mradi huo uliobadilisha mandhari na muonekeno wa eneo lote la stendi kwa kuupa sura ya kisasa ulianza Oktoba, 2020 na kukamilika Oktoba 31, 2022 kwa gharama ya zaidi ya Sh15 bilioni.

Pamoja na mandhari mazuri ya eneo la maegesho ya mabasi na magari madogo, stendi hiyo mpya ambayo ni miongoni mwa vyanzo vya mapapo vya Halmashauri ya Jiji la Mwanza pia ina vyumba vya huduma maalum kwa wasafiri ikiwemo chumba cha faragha kwa ajili ya wanawake wanaonyonyesha.

Stendi hiyo ina uwezo wa kuhudumia mabasi 120 na magari madogo 80 kwa wakati mmoja, vyumba 44 vikubwa vya biashara, maeneo kwa ajili ya mighahawa, mabenki na jengo la abiria.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Juni 6, 2023, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Erick Mvati amesema stendi hiyo imeanza kutumika kwa muda kutoa fursa ya kubaini kasoro na kuyarekebisha kabla ya uzinduzi rasmi.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Sophia Uturo, mmoja wa wasafiri waliokutwa kwenye chumba cha abiria ameipongeza Serikali kwa kuoresha mazingira na miundombinu ya kituo hicho kikuu cha mabasi ambacho ndiyo lango la kuingia na kutoka jijini Mwanza kwa usafiri wa umma kwa njia ya barabara.

"Haya ndiyo matumizi sahihi ya kodi zetu; yaani hapa tunalipa ushuru kwa moyo mkunjufu kwa sababu huduma zimeboreshwa,’’ amesema Sophia

Pongezi kwa Serikali pia zimetolewa na Fred Machibya huku akiishauri Halmashauri ya Jiji la Mwanza kuboresha miundombinu ya barabara zote zinazingia na kutoka ndani ya stendi hiyo ili zilingane na hadhi ya stendi mpya.

"Miundombinu ya barabara, hasa ile ya mabasi madogo maarufu kama daladala bado ni ya hangarawe; ni vema nayo ijengwe kwa kiwango cha lami ili iendane na hadhi ya stendi mpya,’’ amesema Machibya