Sulala la soko liwekewe mkazo kufikia ajenda ya 10/30 – Dk Jacline

Mkurugenzi wa Taasisi inayojishughulisha na Kilimo cha Mbogamboga na Matunda (TAHA), Jacline Mkindi

Muktasari:

Taasisi inayojishughulisha na Kilimo cha Mbogamboga na Matunda (TAHA) imeshauri kuwa suala la masoko linapaswa kuwekewa mkazo katika kuifikia ajenda ya 10/30.

Mbeya. Mkurugenzi waTaasisi inayojishughulisha na Kilimo cha Mbogamboga na Matunda (TAHA), Jacline Mkindi amesema ili kufikia ajenda ya 10/30 jambo muhimu linalotakiwa kuwekewa mkazo zaidi ni suala la masoko.

 Dk Jacline amesema hayo jana, Agost 4, 2022 wakati akijadili kuhusu namna ya kuifikia ajenda hiyo kupitia Kongamano la Kilimo Biashara lililoendeshwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) kupitia Farm Clinic.

“Jambo muhimu sana pamoja na haya yote ni masoko, mie nasema hilo ni namba moja, unajua fedha itakuja tu kama mkulima anapo mahali pa kuuza,” amesema Dk Mkindi.

Amesema kuna haja ya kuboresha na kuweka kipaumbele kwenye mikakati ya kuhodhi masoko ya bidhaa za kilimo kwa kulenga masoko ya Afrika na dunia.

‘Mimi nashauri sekta binafsi zilizo kwenye kilimo kuwa na mkakati wa pamoja wa kuangalia ni jinsi gani tunaweza kujipanga kwenye haya mazao ya kimkakati ili kukamata masoko makubwa kama wanavyofanya wenzetu wanchi jirani,” amesema.

Amesema kwenye mkakati wa kufanya hayo yote kuwa ni endelevu ni lazima Serikali isaidie kutengeneza mazingira wezeshi.

Dk Jacline, amesisitiza suala la kujumuisha pamoja makundi yote muhimu kwenye kuufikia mkakati huo badala ya wadau wa kilimo kujifungia peke yake na kujadili mikakati yao katika kuifikia ajenda ya 10/30.

“Tunapokutana humu kujadili masuala ya kilimo, watu wa afya tunawahitaji, elimu tunawahitaji kwa sababu matatizo ya akili na kilimo yanatokana na namna tunavyofundishwa darasani. Kwa hiyo nafikiri ajenda ya 10/30 sekta ya elimu tuwajumuishe,” amesema Dk Jacline.

Kuhusu suala la banki kuwakopesha wakulima, Dk Jacline alishauri alihoji kama zinaweza kuwakopesha wakulima wanaoanza.

“Hivi mnaweza kuwakopesha wanaoanza?  Tuangalie suala hili, hivi nikiwa na uhakika wa soko, uhakika wa teknolojia kwanini banki isinipe mkopo hata kama naanza kilimo leo kwanini banki msiniamini?” amesema.

Mwisho.