Takukuru yaeleza ilivyomnasa trafiki

Saturday January 22 2022
takukurupic
By Berdina Majinge

Iringa. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Iringa imethibitisha kukamatwa kwa askari wa kikosi cha usalama barabarani, Steven Mchomvu ambaye hivi karibuni aliripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii katika tukio lililomhusisha kupokea rushwa kutoka kwa madereva tofauti.

Kamanda wa Takukuru mkoani Iringa, Domica Mukama alisema Mchomvu alikamatwa Januari 18 kati ya saa tano asubuhi na saa sita mchana, katika eneo la Sido, Ipogolo mjini Iringa na kuwa yupo chini ya uangalizi wa Jeshi la Polisi na atapandishwa kizimbani muda wowote kuanzia sasa.

Akizungumzia tukio hilo jana, Mukama alisema walimkamata trafiki huyo wakiwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kuzuia na kupambana na rushwa mjini Iringa.

“Mtaona katika zile picha zilizosambaa mitandaoni, kuna askari polisi mbali na yule trafiki aliyevaa sare za jeshi hilo, askari huyo ni OCD wa Wilaya ya Iringa. Katika mazingira yale nililazimika kumpigia simu ili tufanye naye kazi kwa pamoja ya kumkamata mtuhumiwa huyo,” alisema.

Alisema trafiki huyo alikamatwa wakati akipokea fedha kutoka kwenye mabasi yaliyokuwa yakipita katika barabara hiyo na kuziweka katika mavazi yake.

“Baada ya kumkamata, tulitaka kujua kutoka kwake ana kiasi gani mfukoni, lakini hakuwa na majibu na ndipo tukamfanyia upekuzi na kukuta akiwa na Sh 152,000,” alisema.

Advertisement

“Kwa polisi wa usalama barabarani na wengine, wasome vizuri mwongozo wa utendaji kazi wao (PGO) ili kujiepusha na vitendo vya rushwa vinavyoweza kuichafua taasisi hiyo nyeti,” alisema.

Alisema wanaendelea kufanya kazi na Jeshi la Polisi na taratibu zote zitakapokamilika, trafiki huyo atapandishwa kizimbani.

Wakati huohuo, kamanda huyo ametoa taarifa ya kazi zilizotekelezwa na taasisi yao katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2021, ikiwamo kudhibiti ubora na ukamilifu wa miradi, yakiwemo madarasa yaliyojengwa kwa fedha za mkopo kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF).

“Jumla ya miradi 12 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Sh7.1 bilioni katika sekta ya elimu, ujenzi na afya ilikaguliwa kwa lengo la kujiridhisha iwapo thamani halisi ya fedha imezingatiwa,” alisema.

Alisema katika kipindi hicho, walipokea malalamiko 48 ambayo kati yake 26 yalihusu rushwa na kufunguliwa majalada, huku uchunguzi wake ukiendelea na mpaka sasa upo katika hatua tofauti.

“Kazi hizo zimetekelezwa ikiwa ni mafanikio ya ushirikiano tunaoupata kutoka kwa wadau mbalimbali katika mapambano ya rushwa,” alisema na kuongeza kwamba wana kesi 10 zinazoendelea kusikilizwa mahakamani.

Kamanda Mukama alisema katika kipindi cha Januari hadi Machi 2022, Takukuru Mkoa wa Iringa imejipanga kuendelea kutatua kero za wananchi zinazohusiana na rushwa na akatoa wito kwa watumishi wa umma kuzingatia miiko ya kazi zao ili kujiepusha na vitendo hivyo vinavyoweza kuwaingiza matatani.

Advertisement