Takukuru yakagua miradi 42, minne inamapungufu Mwanza

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, James Ruge akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza

Muktasari:

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Mwanza imekagua na kufuatilia miradi 42 inayogharimu zaidi ya Sh26 bilioni kwa kipindi cha Januari hadi Machi, 2023.

Mwanza.Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Mwanza imekagua na kufuatilia miradi 42 inayogharimu zaidi ya Sh26 bilioni kwa kipindi cha Januari hadi Machi, 2023.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Mei 26, 2023, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, James Ruge amesema kati ya miradi hiyo miradi minne katika sekta ya Afya, Elimu na Maji iliyogharimu zaidi ya Sh3 bilioni ilikutwa na mapungufu na wahusika kutakiwa kurekebisha mapungufu hayo.

Ruge amesema katika jukumu la kuzuia rushwa, wametekeleza program ya ‘Takukuru rafiki’ ili kuongeza ushiriki wa kila mwananchi na wadau kukabiliana na rushwa kwenye utoaji huduma za jamii na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Amesema jumla ya Kata 14 za Mkoa wa Mwanza zilifikiwa na program hiyo ambapo vikao kati ya taasisi hiyo na wananchi vilifanyika na kubaini changamoto mbalimbali kisha kukaa na watoa huduma ili kutatua changamoto hizo.

Amesema miongoni mwa kero walizobaini ni wajawazito na wazee kutozwa fedha kwenye vituo vya kutolea huduma za afya katika Kata ya Fumagila ili wahudumiwe hata hivyo, amesema kwa sasa changamoto hiyo imetatuliwa kwa walezi wa vituo hivyo kuvitembelea kila wiki na kutoa taarifa kwa Mganga Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana.

“Katika kutoa elimu kwa umma, semina 59 zimetolewa kwa watumishi wa umma na sekta binafsi, mikutano ya hadhara 69 imefanyika kwa wananchi katika ngazi ya Kata, Mitaa na Vijiji huku Klabu za wapinga rushwa 170 katika shule za msingi, sekondari na vyuo zikiimarishwa,”

“Katika kipindi cha Januari hadi Machi, 2023 Takukuru imepokea taarifa 90 kati ya taarifa hizo, taarifa 81 zinahusu vitendo vya rushwa na taarifa tisa hazihusu vitendo vya rushwa. Uchunguzi wa taarifa 81 za rushwa unaendelea,”amesema Ruge

Amewataka viongozi na watumishi wanaotumia nafasi zao kujinufaisha kwa njia za rushwa kuacha tabia hiyo badala yake wawajibike kwa nafasi zao na kuwa msatari wa mbele kuzuia na kukemea rushwa huku akiwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano ili kupambana na vitendo hivyo.